Habari za Kaunti

Wakeketaji waficha uovu wao kwa muziki wa juu

February 29th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

HUKU Kenya na ulimwengu ukiendeleza kampeni dhidi ya ukeketaji, tatizo hilo bado linaendelea kukithiri na kukita mizizi miongoni mwa jamii za baadhi ya miji na vijiji vya Lamu.

Imebainika kutoka kwa maafisa wa utawala wa serikali kuu na wanaharakati kuwa vijiji vingi, hasa vile vya jamii za wafugaji, Kaunti ya Lamu, vimekuwa vikiibuka na mbinu mbalimbali za kuendeleza tohara ya mwanamke, ilmradi serikali na wadau wanaopinga uozo huo katika jamii wasijue kamwe.

Miongoni mwa mbinu hizo ni ile ya wakeketaji kutumia muziki, ambapo wamekuwa wakiweka midundo mikalimikali nje ya nyumba zao utadhani kuna sherehe kubwa inaendelea ilhali ukeketaji, hasa kwa wasichana wadogo, ukiendelezwa chini kwa chini kwa wakati huo.

Baadhi ya sehemu zilizotajwa kuendelezwa maovu hayo ni Witu Mjini, Koreni, Pangani, Mokowe, Dide Waride, Kitumbini, Chalaluma, Moa, Nairobi Area, Vipingoni, Onido, Pandanguo, Jima, Lumshi, Bar’goni, na viunga vyake.

Maeneo hayo ni ngome kuu za jamii za wafugaji, hasa Orma, Wasomali, Waborana, Waata (Watha) na Waboni.

Katika mahojiano na Taifa Leo, mwanaharakati wa kampeni za kukabiliana na ukeketaji, Kaunti ya Lamu, ambaye pia jamii yake imeathiriwa na uovu huo, Bi Zainabu Gobu Wako, alikiri kusheheni kwa tabia hizo alizozitaja kupitwa na wakati.

Bi Gobu anatoka jamii ya Orma wanaoishi Witu.

Kutokana na kukithiri kwa ukeketaji vijijini, Bi Gobu ameunda na kuibuka na vuguvugu au muungano kwa jina Lamu Women Femi Sight, dhamira kuu ikiwa ni kupigana na ukeketaji na dhuluma zingine za kijinsia, hasa wanawake, Kaunti ya Lamu.

Bi Gobu alifichua kuwa jamii nyingi eneo hilo zimekuwa zikiwalenga wasichana wa umri mdogo, ambao ni wa kati ya miaka mitano na saba, ambapo wamekuwa wakiwashurutisha kutahiriwa wakijua fika kuwa watoto hao hawana nguvu yoyote ya kujitetea.

“Utapata nyakati za likizo wasichana wengi wadogo humu vijijini mwetu wakipitia kisu cha ngariba. Jamii inajua kabisa serikali na wakereketwa wa haki wanapinga tabia hiyo ya kukeketa. Kwa sababu hiyo, wengi sasa wameibuka na mtindo wa kuweka midundo au muziki wa juu nje ya majumba yao. Utapata hata watoto wengine  wakicheza densi hiyo utadhani kuna sherehe ya nikaha ama matanga. Baadaye ndipo unagundua kumbe kulikuwa na visichana au vitoto vidogo vilivyokuwa vimefichwa ndani kukeketwa,” akasema Bi Gobu.

Afisa na mwanaharakati wa kampeni dhidi ya ukeketaji kwa jina Lamu Women Femi Sight, Zainabu Gobu Wako akihutubia wanahabari ambapo alisema muziki wa juu umekuwa ukitumiwa na wakeketaji kuficha vitendo vyao dhidi ya wasichana. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema kucheza muziki wa juu ni harakati za kuficha wale watakaolemewa na kisu cha ngariba na kupiga kelele.

“Yaani kwa wale watakaopiga kamsa kutokana na maumivu basi wasitambuliwe kwani muziki huwa umetamalaki hewani. Hata ukalia ni kazi bure kwani huwezi ukasikika kamwe,” akasema Bi Gobu.

Aliisihi serikali kuzidisha operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wanaoendeleza maovu hayo endapo ina nia ya  kufaulisha vita dhidi ya ukeketaji miongoni mwa jamii ya Lamu na nchini kwa ujumla.

Pia aliomba mashirika ya kijamii yaliyojitolea kukabiliana na ukeketaji kuwezeshwa kupitia ufadhili mbalimbali.

“Sisi kama wanaharakati punde tunapowezeshwa itatupa uwezo wa kutembea miji na vijijini kuhamasisha umma kuhusiana na athari za ukeketaji,” akasema Bi Gobu.

Bw Yusuf Ali, ambaye pia ni mpingaji mkuu wa tohara ya wanawake, alieleza masikitiko yake kuhusiana na jinsi itikadi hiyo ya kukeketa wasichana inavyochangia ndoa na mimba za mapema na ongezeko la idadi ya wanaoacha shule eneo hilo.

“Punde msichana anapokeketwa inamaanisha yuko tayari kuolewa na kuanza maisha ya utu uzima bila kujali umri wake. Wasichana wetu wengi hapa wameacha shule punde wanapokeketwa ilhali wengine wakiishia kuolewa. Lazima tabia hii ikomeshwe,” akasema Bw Ali.

Naibu Kamisna wa taarafa ya Witu Emmanuel Wesley Koech, alikiri kusheheni kwa ukeketaji miongoni mwa jamii, hasa za eneo lake, akisema serikali inaendeleza msako mkali dhidi ya wahusika.

Wanawake kutoka jamii za wafugaji wa Lamu Magharibi wakati wa kongamano lao kwenye ukumbi wa kijamii wa Witu. Ukeketaji bado ni changamoto kwa jamii za Witu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alitaja wasichana wadogo wa umri wa kati ya miaka minane, kumi na mbili na kumi na tano kuathiriwa pakubwa na ukeketaji eneo hilo.

“Tayari tumeshika watu kadhaa kutoka kijiji cha Vipingoni, ikiwemo mzee mmoja na mama. Walikuwa wametekeleza ukeketaji wa wasichana watatu wadogo na kuwaachia majeraha mabaya karibu wafe. Kwa sababu wamefahamu kwamba serikali iko macho kukabiliana na ukeketaji, wanajamii sasa wamekuwa wakiwahamisha wasichana wao kuwafanyia tohara kisiri kaunti jirani ya Tana River. Tuko chonjo na lazima tukomeshe kabisa tamaduni hii potovu na iliyopitwa na wakati,” akasema Bw Koech.

Naibu Kamishna wa tarafa ya Witu Emmanuel Wesley Koech akihutubia wanahabari. Aliasema tayari wamekamata watu kadhaa kuhusiana na vitendo vya kuwakeketa wasichana. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa athari za ukeketaji ni wahasiriwa kukumbwa na matatizo ya kisaikolojia, ikiwemo msongo wa mawazo, wasiwasi, kupata kiwewe baada ya kujifungua na kutojiamini.

Wahasiriwa pia hupata matatizo wakati wanaposhiriki tendo la ndoa, ambapo mara nyingi huhisi maumivu wakati wa tendo, kutofurahia tendo na kutoridhika au kufika kileleni.

Kuna wanaoshuhudia mshtuko na hata kifo wakati wakipitia ukeketaji.