Habari za Kitaifa

Wakenya 14 waokolewa kutoka kwa genge la ukahaba India


POLISI nchini India wamewaokoa wanawake 17 wa asili ya nchi za Afrika Mashariki kutoka kwa genge linaloendesha biashara ya ukahaba nchini humo na kuwatia mbaroni washukiwa watatu wa uovu huo.

Idara ya Polisi ilisema Wakenya 14, Waganda wawili na Mtanzania mmoja ni miongoni mwa wale waliookolewa Ijumaa baada ya maafisa wa usalama kuvamia jumba moja la ghorofa tatu.

Kulingana na chapisho moja nchini India, Polisi wa Kitengo cha Kupambana na Ulanguzi wa Binadamu walivamia jumba moja katika kitongoji cha Kondapur, wilaya ya Hyderabad na kuwakamata washukiwa watatu waliotuhumiwa kupanga sakata hiyo.

Idara ya Polisi ilisema kiongozi wa genge hilo la raia wa kigeni huendesha shughuli zao mitandaoni.

“Alibuni sehemu katika mtandao wa “Locanto” ambako alipitisha jumbe kuhusu biashara haramu ya ukahaba. Wanawake hao wanaotumiwa katika uovu huo wamekuwa wakizungushwa katika miji kadhaa kama vile Delhi, Mumbai, Bengaluru na Hyderabad,” taarifa ya polisi ilisema.

Kulingana na polisi, wanawake hao waliwasili India wakitumia visa zilizoonyesha kuwa wao ni watalii au watu waliofika India kusaka huduma za matibabu.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake waliendelea kuishi India baada ya muda wa matumizi ya visa zao kuisha.

Inakadiriwa kuwa genge hilo la kuendesha sakata ya ukahaba hukusanya kati ya Sh4,602 na Sh30, 682 kutoka kwa wateja.

Polisi walinasa simu nne za mkononi, mipira 104 za kondomu, vifaa vya kupima virusi vya HIV na vifaa vya ngono.

Washukiwa hao watatu walisukumwa kwenye rumande ya polisi na wanawake hao 17 wakapelekwa katika makao ya kuhifadhi watu waliookolewa kutoka kwa mateso.

Wanawake hao waliokolewa siku chache baada ya serikali ya Kenya kuonya raia wake dhidi ya ahadi bandia za ajira katika mataifa ya Kusini mwa bara Asia, ikiwemo nchini Myanmar, ambamo wameishi kutumika kama watumwa.

Kulingana na notisi moja ya serikali iliyotolewa Agosti 16, Wakenya kadhaa na raia wengine wa mataifa ya Afrika Mashariki wamevutiwa kuenda nchi za Myanmar, Laos na Cambodia kufanya kazi kama walimu wa lugha ya Kiingereza. Lakini wanaishi kufanyishwa kazi kwa muda mrefu kwa mapato duni.

Onyo la hivi punde lilitoka katika Ubalozi wa Kenya nchini Thailand baada Mkenya mmoja kufa hospitalini.

Ubalozi huo ulisema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa haswa baada ya wanaoendesha shughuli ya kuwaita Wakenya waende Thailand kutumia Wakenya wengine kuwarai wenzao wakiwaahidi nafasi hewa za ajira.

Ubalozi wa Kenya ulisema juzi ilishirikiana na asasi mbalimbali kuokoa zaidi ya Wakenya 140 na watu wengine wa asili ya nchi za Afrika Mashariki.

Hii inaonyesha kuwa mwenendo wa kuwavutia Wakenya kusafiri hadi Thailand umekuwa ukiendelea licha ya onyo kutoka kwa ubalozi huo tangu mwaka wa 2022.