Michezo

Wakenya 2 wajishindia tiketi ya kutazama Kombe la Dunia Urusi

May 21st, 2018 2 min read

Afisa Mkuu wa Biashara ya Mauzo wa KCB Wanyi Mwaura (katikati) akipiga picha na washindi wa shindano la ‘KCB Visa World Cup promotion’. Kutoka kushoto ni Samson Okoth na mwanawe Gershom Okoth, na Esther Warui na mumewe Willy Wainaina (kulia). Picha/ Geoffrey Anene

Na GEOFFREY ANENE

SAMSON Okoth na Willy Wainaina wameibuka washindi wa shindano la ‘KCB Visa World Cup promotion.’

Wamejishindia safari ya kuenda nchini Urusi iliyolipiwa kila kitu kutazama Kombe la Dunia litakaloanza Juni 14 na kutamatika Julai 15 mwaka 2018. Watatazama mechi ya ufunguzi kati ya Urusi na Saudi Arabia uwanjani Luzhniki jijini Moscow.

Wawili hawa, ambao ni wateja wa Benki ya KCB, wataruhusiwa kuandamana na mtu mmoja zaidi kutoka familia zao kwa burudani hili.

Okoth atasafiri na mtoto wake wa kiume Gershom Okoth,22, ambaye ni mchezaji wa timu ya Strathmore University, naye Wainaina ameamua kuzuru Urusi na mkewe Esther Warui, ambaye ni mama wa watoto wawili.

Akizingumza katika hafla ya kutangaza washindi, Afisa Mkuu wa Biashara ya Mauzo wa KCB Wanyi Mwaura alipongeza wawili hao kwa kujishindia safari hiyo ya Urusi na kuongeza kwamba KCB inafurahia kuwapa wateja wake uhondo kamili katika ulingo wa dunia wa soka.

“Ningependa kuwapongeza nyinyi na familia zenu kwa kushinda safari hii ya kipekee na ninawaombea safari njema na nawapongeza tena kwa kuamini bidhaa zetu,” alisema Wanyi.

Okoth, ambaye ni mhadhiri wa masuala ya usoroveya katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) alitumia kadi ya benki (KCB Visa Card) kununua gazeti na vyakula vya familia.

Washindi hawa wamelipiwa nauli ya ndege ya kuenda Urusi na kurudi. Nauli ya chini ya ndege kutoka Nairobi hadi Moscow ni Sh77,191. Kutoka Moscow hadi Nairobi, nauli ya chini ni Sh55,984.

Vilevile, wamejishindia tiketi za sehemu nzuri ya kutazama mechi (Category 1) ambazo pia zinaandamana na mapokezi ya hali ya juu.

Bei ya tiketi hizi za kundi la kwanza ni kati ya Sh20, 241 na Sh106,028 kila moja. Wamiliki wa tiketi hizi wanakaa katika sehemu nzuri ya uwanja. Sehemu hizi haziko nyuma ya goli. Zinapatikana sana upande mrefu wa uwanja. Pia wamelipiwa siku nne kuishi katika hoteli ya kiwango cha juu cha ‘Nyota Tano’ ya Marriot jijini Moscow pamoja na bidhaa zingine za kupendeza.

Wainaina anafanya kazi ya utalii katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi. Yeye ni shabiki sugu wa klabu ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.