Habari MsetoSiasa

Wakenya 4 wamefanikiwa kupenya Ikulu tangu Uhuru aingie madarakani

June 11th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

KISA cha mwanafunzi wa JKUAT, Brian Kibet Bera kuvamia Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatatu jioni ni cha nne kwa raia kuingia Ikulu bila idhini tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoingia mamlakani.

Kisa kimoja kilishuhudiwa 2016 wakati mwendeshaji mkokoteni, Bw William Ngene alipokamatwa baada ya kuruka kuta mbili na kuingia Ikulu.

Alipofikishwa mahakamani, alisema yeye huona tu Ikulu kwenye picha na televisheni, ndiposa akatamani sana kujionea kwa macho. Siku chache baada ya korti kumwachilia huru, alipatikana amefariki Uhuru Park katika hali zisizoeleweka akiwa na jeraha kichwani.

Kisa cha kutisha zaidi kilitokea 2017 pale mwanamume alipopigwa risasi na maafisa wa GSU akafariki.

Hii ilikuwa mara ya kwanza katika historia kwa mtu kuuawa ndani ya Ikulu. Polisi walisema alikuwa peke yake akizurura ndipo akapigwa risasi mara tatu.

Mnamo 2015, Walter Juma alikamatwa Ikulu na akapelekwa kuhojiwa na kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi. Alipofikishwa mahakamani alisema haikuwa mara yake ya kwanza kuingia Ikulu na akadai Rais Kenyatta ni rafiki yake.

Tawala za marais wastaafuu Mwai Kibaki na Daniel arap Moi pia zilikuwa na visa aina hii. Mnamo 2004 wakati Mzee Kibaki alipokuwa mamlakani, raia wa Australia alipatikana Ikulu rais alipokuwa akila kiamsha kinywa.

Mnamo 2002, Onyango Mono alikamatwa ndani ya Ikulu akiwa amelala kwenye zulia. Iliaminika aliingia humo jioni lakini walinzi walimpata tu asubuhi.

Alidai alikuwa ametumwa na Mungu kumwambia Mzee Moi aondoke mamlakani mara moja.