KimataifaSiasa

Wakenya Amerika wagawanyika wamchague Trump au Joe Biden

November 1st, 2020 3 min read

Na CHRIS WAMALWA akiwa Amerika

BI Pauline Ochieng yuko mbali mno kutoka nyumbani kwao Seme, Kisumu alikozaliwa. Lakini mama huyo aliye na watoto wawili na sasa ni Mwamerika, anatambua kwamba, mtaa wa Garden Estate katika jimbo la New Jersey ndipo nyumbani kwa sasa.

Anahimili baridi kali asubuhi eneo la Basking Ridge kupiga kura ya mapema ya urais. Chaguo lake ni mgombeaji wa chama cha Democrat, Joe Biden.

“Najua hili ni jambo ambalo limesemwa sana, lakini wacha niseme, kila kura ni muhimu. Ninapiga kura kwa sababu Amerika iko kwenye njiapanda. Rais Donald Trump ni tishio kwa demokrasia ulimwenguni,” Bi Ochieng aliambia Taifa Jumapili katika mahojiano.

Kando naye, Bw Patrick Odoyo, mzaliwa wa Kenya ambaye sasa anaishi Orlando, Florida, pia amepiga kura yake katika jimbo hilo ambalo hung’ang’aniwa na wanaoshindania urais.

“Sikutaka kubahatisha. Chochote chaweza kufanyika siku ya uchaguzi, kama vile hali mbaya ya hewa ama milolongo mirefu kupita kiasi. Nilitaka kuhakikisha nashiriki katika uchaguzi huu,” akasema kwenye mahojiano ya simu.

Bi Ochieng na Bw Odoyo ni miongoni mwa maelfu ya Wakenya waliopata uraia Amerika ambao wamejiunga na idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo kupiga kura zao mapema kabla uchaguzi wa urais ufanyike Jumanne.

Tofauti na zamani, Wakenya kiasi kikubwa ikilinganishwa na zamani wameondoa uaminifu wao kwa wagombeaji wa Democrat, ambao ni Biden na mgombea mwenzake Kamala Harris.

Sawa na jinsi ilivyo nchini Kenya, siasa ni jambo lenye mvutano miongoni mwa Wakenya wanaoishi Amerika.Huku nchini Kenya wananchi wakigawanyika kwa misingi ya kikabila katika siasa, nchini Amerika huwa wamegawanyika kwa misingi ya kidini.

“Huwezi kuelewa migawanyiko inayokumba Wakenya wanaoishi hapa kama wewe si mmoja wao. Huwa wanaficha uhasama wao kuhusu masuala ya uchaguzi na siasa za Democrat dhidi ya Republican,” akasema Prof Joseph Situma wa Chuo Kikuu cha Wilmington kilicho Delaware.

“Huwa inaaminika kwamba Wakenya wataunga mkono mgombeaji wa Democrat, lakini ukweli ni kwamba kuna idadi yao kubwa ambao ni wafuasi wa Republican na walimpigia kura Trump, bila kujali misimamo yake kuhusu raia wa kigeni,” akaeleza.

Bw James Sang, mkazi wa Baltimore, Maryland, alisema ingawa Wakenya wengi na Waafrika kwa jumla ni waumini wa dini na wenye misimamo mikali ya kitamaduni, huwa wana uhuru wa mawazo kuhusu masuala mengine ya kijamii.

“Haswa, huwa wanazingatia misimamo ya Waamerika wanaoshikilia imani za kidini ambao hupinga masuala kama vile ushoga, uavyaji mimba na mengineyo. Lakini kisiasa, wanaunga mkono wale wenye uhuru wa kimawazo, ambao filosofia yao ni kuhusu haki za kijamii na usawa,” akasema Bw Sang.

Mtaalamu huyo wa masuala ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano alisema kijumla, Waafrika hupenda ujamaa, kuhusu ugavi sawa wa rasilimali.

Ni katika hali hii ambapo wao hutofautiana na Waamerika wanaotetea ubinafsi.“Ujamaa wa Waafrika unawiana vyema sana na misimamo ya Chama cha Democratic, kuhusu uhuru, usawa wa kijamii, marekebisho ya sera zinazohusu raia wa kigeni na upanuzi wa mipango kama vile elimu ya juu ya gharama nafuu na huduma nafuu za afya,” akasema.

Dkt David Amakobe, ambaye ni mtaalamu wa tabia za binadamu kutoka Middletown, Delaware, anaamini kuna jambo jingine linalofanya wahamiaji kuamua kumpigia kura Biden.

Kulingana naye, Trump ni kiongozi mbaya ambaye sera zake zimeathiri sana wahamiaji.Anaongeza kuwa, wahamiaji wanajiona kama kwamba watakubalika zaidi katika utawala wa Biden na Harris kwa sababu kuna idadi kubwa ya Waafrika katika kikosi chake cha kampeni ambao wanaweza kufanya maamuzi kuhusu sera.

“Sisi sio tu kikundi cha wafanyakazi wageni wanaoshukuru Amerika kwa kutukubali na wanaotafuta misaada. Sisi ni walipa ushuru ambao wanataka uwajibikaji kutoka kwa viongozi tunaowachagua. Tunataka suluhisho kwa changamoto zilizopo kabla tuzungumzie sera za mahusiano ya nchi za kigeni,” akasema.

Dkt Amakobe ambaye ni mwanachama wa Democrat eneo la Delaware, ni miongoni mwa kikundi kidogo cha wahamiaji ambao walishinikiza kikosi cha kampeni za Biden na Harris kuweka ajenda maalumu ya Waafrika waliopata uraia Amerika, ambayo sasa imetangazwa miongoni mwa ajenda muhimu katika tovuti ya chama hicho.

“Kampeni tunayowafanyia Biden na Harris si kwa vile ni malaika na tunawapenda, bali ni kwa kuwa tuna ajenda na tuna nafasi katika meza yao kuishinikiza ajenda hiyo,” akasema Dkt Amakobe katika mahojiano na Taifa Jumapili.

Ajenda hiyo inatambua kuwa Waafrika wanaoishi Amerika ni mojawapo ya jamii kubwa yenye lugha tofauti ambao ni wa matabaka tofauti ya kijamii, walio na imani tofauti.

Sehemu ya maelezo kuhusu ajenda hiyo inasema ingawa Waafrika wanatofautiana kwa masuala mbalimbali, wao wana msimamo sawa katika mambo mengi ikiwemo kitamaduni na kimaadili hasa katika masuala ya kusaidia familia zao, kutoa nafasi sawa kwa jamii na kuchangia kwa ukuaji na ustawishaji wa Amerika.

“Joe Biden na Kamala Harris wamekubali ajenda hii na ninafahamu kuwa utawala ujao lazima uelewe kile ambacho utawala uliopo hauelewi. Nchini Amerika, haijalishi mahali ulianzia maisha yako wala mahali wazazi wako walizaliwa. Hakufai kuwa na vikwazo kwa mafanikio yako wala kile unachoweza kutimiza. Wakiwa rais na naibu rais, Joe Biden na Kamala Harris watajenga upya nchi yetu kwa njia inayoleta pamoja kila mtu,” sehemu ya ajenda hiyo inasema.