Habari Mseto

Wakenya asilimia 67 wanaamini ufisadi umeongezeka nchini – TI

December 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wengi bado wanaamini kuwa visa vya ufisadi vimeongezeka nchini wakati huu wa janga la corona, kulingana na shirika la kimataifa la kuchunguza ufisadi, Transparency International, tawi la Kenya.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Sheila Masinde alisema asilimia 67 wangali wanaamini kuwa ufisadi umekithiri zaidi haswa katika sekta ya umma huku Kenya ikiorodheshwa nambari 137 miongoni mwa mataifa 180 fisadi zaidi ulimwenguni.

“Hii ina maana kuwa Kenya bado haifanyi vizuri katika vita dhidi ya ufisadi. Uovu huu bado umekithiri haswa miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu serikalini. Kesi za ufisadi nazo zingali zinajivuta mahakamani,” akasema Jumatatu usiku kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa asasi za kupambana na ufisadi kubuni mbinu mbadala za kuharakisha kesi za ufisadi haswa zinazowahusu mawaziri, magavana, wabunge na maafisa wengine wenye vyeo vya juu serikali.

Bi Sheila alisema hayo huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Uhamasisho Dhidi ya Ufisadi Jumatano, Desemba 9, 2020.

Hata hivyo, Kamishna wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Mwaniki Gachoka alisema ufanisi katika vita dhidi ya ufisadi unahitaji ushirikiano katika wa Wakenya na asasi zote humu nchini.

“Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeshughulikia zaidi ya kesi 800 za ufisadi zinazowahusu maafisa wa vyeo juu serikalini na katika sekta ya kibinafsi. Baadhi yao wamefunguliwa mashtaka kortini kwa misingi ya ushahidi tuliopata,” akasema.

Bw Gachoka aliongeza kuwa kufikia sasa tume hiyo imekomboa Sh20 bilioni zilizoporwa kupitia sakata kadha za ufisadi, akisema hiyo ni ishara kuwa juhudi za EACC za kupambana na uovu huo zinazaa matunda.

“Kando na hayo, wakati huu tume inafuatilia mali ya thamani ya Sh23 bilioni zilizopatikana kwa njia ya ufisadi,” akaeleza.

Kuhusu sakata ya Sh7.8 bilioni iliyozonga Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) Bw Gachoka alisema kuwa wakati huu tume hiyo inachunguza kampuni 80 zilizodaiwa kuhusika katika sakata hiyo.

“Ingawa siwezi kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hili kwa sababu uchunguzi ungali unaendelea nchini na ng’ambo, tutawasilisha ushahidi wetu kwa asasi husika baada ya kukamilisha uchunguzi,” akasema.

Sakata hiyo ambayo pia ingali inachunguzwa na Kamati ya Seneti kuhusu Afya ilichangia kuachishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kemsa Jonah Manjari na maafisa wengine wakuu wa asasi hiyo.