Habari

Wakenya bado mateka kisiasa

September 12th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MATUKIO ya wananchi kufuata wanasiasa kikondoo kwa kiasi cha kushambuliana hadharani, yameanza kuibuka huku wanasiasa wakijitafutia umaarufu kabla Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka wa 2022.

Tangu jadi, viongozi wa kisiasa nchini wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali kuwarai wananchi wawaamini kwa kiasi cha kujitolea mhanga, lakini baadaye ahadi za viongozi kwa raia hugeuka kuwa hewa na zisizotimika.

Ijumaa, kulitokea visa kadha vya maandamano ya wananchi waliodai kuwatetea wanasiasa.

Mamia ya wananchi waliungana na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kwa maandamano ya kukashifu serikali kwa ‘ubaguzi wa kisiasa’ mjini Eldoret. Bw Sudi anaandamwa na madai ya uchochezi wa kijamii.

Katika eneo la Emurua Dikirr, mamia wengine waliandamana na Mbunge Johanna Ng’eno ambaye alikuwa ameondoka kituo cha polisi. Alikuwa amezuiliwa kwa madai ya uchochezi.

Wakati huo huo, polisi walilazimika kurusha vitoa machozi kutawanya kikundi cha vijana kilimshambulia Mbunge wa Igembe Kusini, Bw John Paul Mwirigi.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Kanuni, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kilimo cha alizeti. Hafla hiyo ilikuwa imehudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya.

Mnamo Alhamisi, makabiliano mabaya yalitokea kati ya wandani wa Naibu Rais William Ruto na wale wanaounga mkono handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Kaunti ya Kisii.

Matukio mengine kama haya yaliyotokea awali ni maandamano wakati viongozi wanapokamatwa kwa sababu ya madai mbalimbali ikiwemo ufisadi na uchochezi wa jamii.

Katika hotuba yake Kisii, Dkt Ruto aliungama kuwa tabia ya wananchi kuchochewa na wanasiasa imepitwa na wakati.

“Kuna wengine wanaofikiri kutakuwa na fujo tena. Wajinga wa kupigana hawako tena na Kenya itakuwa na amani kwa sababu sisi sote tuko chonjo,” akasema.

Bw Okeng’o Nyambane, ambaye ni mwenyekiti wa vijana kutoka eneobunge la Kitutu Chache Kusini, alisema wanasiasa wanafaa kuwaheshimu vijana na badala ya kuwatumia ili kuleta fujo, wanafaa kuyashughulikia maswala yanayowakumba vijana kama vile ukosefu wa ajira.

Kwa mujibu wa Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, imekuwa kawaida kwa wanasiasa nchini kujipendekeza kwa raia kwa kila njia ikiwemo kwa kujionyesha kuwa mmoja wao kimaisha.

Hii ni mojawapo ya sababu zinazoaminika kufanya raia kuwafuata bila kujali hatima yao wenyewe, kando na madai ya wanasiasa kufadhili vijana ili watekeleze yale yote wanayotaka ikiwemo kuzua fujo.

Kijumla, wadadisi wanasema kuwa pigo kuu limekuwa kwa wananchi wenyewe, kwani wanasiasa wengi husahau ahadi ambazo hutoa kwao wakati wanapowarai kuwapigia kura.

Wanatoa mfano wa utawala wa Jubilee, ambao umekosa kutimiza ahadi nyingi uliotoa kwenye kampeni zake mnamo 2013 na 2017 mtawalia.

Wadadisi walieleza kuwa, mbinu ya wanasiasa kujileta chini hadi wananchi waamue ni wenzao zilianza kutumiwa zamani hasa wakati wanasiasa kama vile Jaramogi Oginga Odinga na Kenneth Matiba walikuwa wakikabiliana na udhalimu wa serikali ya marehemu Daniel arap Moi.

“Wakati huo, Bw Matiba na wanasiasa wengine wa upinzani kama Jaramogi, walijisawiri kama “mashuja na watetezi wa raia” ili kujipa umaarufu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba lengo lao kuu lilikuwa kumshinda Moi,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri wa Historia.

Hata hivyo, Dkt XN Iraki, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi, anasema wanasiasa wanapokosa kuoanisha ahadi za kisiasa na hali ya kiuchumi ya nchi ndipo wanaishia kuwahadaa wananchi.

Anasema wengi husahau kuwa utekelezaji wa ahadi hizo huhitaji sera, fedha na mikakati mingi ya wataalamu na washauri wa kiuchumi.

“Hilo ndilo wanasiasa wengi husahau. Ni kosa ambalo huja kuligundua baadaye wanapobaini kwamba uchumi na mapato ya nchi hayawezi kufadhili hata nusu ya ahadi walizotoa,” akasema mtaalamu huyo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Bw Wilson Sossion, anasema kuwa kosa kuu la wanasiasa ni kukosa kuwashirikisha wadau katika sekta husika wanapobuni manifesto zao.

Ripoti za Wanderi Kamau, Wycliffe Nyaberi, David Muchui na Vitalis Kimutai