Habari

'Wakenya hawatatumika kama 'wanyama' wa kufanyia majaribio chanjo dhidi ya Covid-19'

April 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali madai kwamba Kenya imewaruhusu watafiti kutoka Uingereza kuifanyia majaribio chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa Covid-19 nchini.

Kwenye hotuba yake kwa taifa, kiongozi wa taifa alibainisha hakuna mipango yoyote ya wanasayansi kutoka nje kuja nchini kuwatumia Wakenya kuifanyia majaribio chanjo ya corona.

“Kile tunajua ni kwamba Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Nchini (Kemri) inashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa katika mchakato wa kusaka dawa au chanjo dhidi ya corona. Tutafuata mwelekeo kutoka kwa taasisi hiyo kuhusu suala hili muhimu wala sio watu wengine kutoka nje,” Rais Kenyatta akasema katika Ikulu ya Nairobi Jumamosi.

Akaongeza: “Ningependa kuwahakikishia kuwa ripoti zinazosambazwa kwa vyombo vya habari kuhusu mipango ya majaribio ya chanjo ni uongo. Wanasayansi na watafiti wanaendelea kutafuta chanjo na wakipiga hatua yoyote tutawafahamisha. Hatutafanya kitu chochote pembeni au kwa siri.”

Mnamo Ijumaa, Shirika la Habari la Uingereza (BBC) lilitangaza kuwa watafiti kutoka Uingereza wameteua Kenya kuendeshea majaribio ya chanjo dhidi ya Covid-19.

Hii ni ikiwa majaribio yatakayoendeshwa nchini Uingereza hayatatoa matokeo yanayotarajiwa.

Majaribio ya kwanza ya chanjo dhidi ya virusi vya corona katika bara Uropa yalianza Alhamisi.

Wawili miongoni mwa watu 800 waliojitolea kwa majaribio hayo walipewa chanjo hiyo iliyotengenezwa na kundi la wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.

Utafiti huo uliongozwa na Profesa Sarah Gilbert ambaye ni mtaalamu wa fani ya chanjo katika Taasisi ya Jenner.

Nusu ya watu hao waliojitolea watapewa chanjo dhidi ya virusi vya corona ilhali waliosalia watapewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa utandu wa mgongo, yaani meningitis.

Haya yanajiri wakati ambapo serikali ilithibitisha visa vingine saba vya maambukizi ya virusi vya corona, na kufikisha idadi jumla ya visa hivyo nchini kuwa 343 kufikia Jumamosi.