Michezo

Wakenya Jepchirchir na Chebet washinda Valencia Marathon

December 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKENYA Peres Jepchirchir na Evans Chebet ndio mabingwa wapya wa Valencia Marathon kwa upande wa wanawake na wanaume mtawalia.

Wawili hao walitawala kategoria zao katika mbio hizo mnamo Disemba 6, 2020 na kusajili rekodi mpya.

Jepchirchir ambaye alikuwa kishiriki mbio za kilomita 42 kwa mara ya kwanza aliweka historia ya kuwa mwanariadha wa nane kuwahi kukamilisha mbio za marathon chini ya kipindi cha saa mbili na dakika 18 alipofika utepeni baada ya muda wa saa 2:17:16.

Mtimkaji huyo ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za nusu marathon, anakuwa Mkenya wa kwanza kuwahi kushinda mbio za Valencia Marathon baada ya Valary Ayaibei mnamo 2016.

Muda aliousajili jana ulifuta rekodi ya saa 2:18:30 iliyowekwa na Mwethiopia Roza Dereje katika mbio za Valencia Marathon mnamo 2019.

Kwa upande wake, Chebet alimduwaza bingwa wa Boston na Chicago Marathon, Lawrence Cherono aliyepigiwa upatu kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume.

Chebet alimzidi Cherona maarifa katika hatua ya mita 800 za mwisho na kukata utepe baada ya saa 2:03:00. Muda huo ulifuta rekodi ya awali ya saa 2:03:51 iliyowekwa na Mwethiopia Kinde Atanaw katika Valencia Marathon mnamo 2019.

Mwethiopia Birhanu Legese ambaye ni bingwa wa Tokyo Marathon aliambulia nafasi ya tatu baada ya muda wa saa 2:03:16.

Mshindi wa nishani ya shaba katika marathon ya dunia, Mkenya Amos Kipruto aliridhika na nafasi ya nne baada ya kusajili muda bora wa saa 2:03:30.