Michezo

Wakenya kujaribu kutwaa taji Nagoya Marathon

February 26th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI Lucy Kabuu, Valary Jemeli na Flomena Cheyech Daniel watashiriki Nagoya Marathon hapo Machi 11 nchini Japan kila mmoja akitafuta kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa taji tangu mbio hizi zianzishwe mwaka 1980.

Kabuu, 33, alisomea shule moja ya upili nchini Japan kabla ya kujitosa katika mbio za barabarani, lakini hajakamilisha mashindano ya kilomita 42 tangu amalize Dubai Marathon katika nafasi ya tatu mwaka 2015 kwa saa 2:20:21.

Cheyech, 35, anafahamu nchi ya Japan vyema sana kwa sababu yeye pia aliwahi kuishi humo. Bingwa huyu wa marathon kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2014 alinyakua mataji ya Saitama Marathon nchini Japan mwaka 2016 na 2017.

Naye Jemeli hajawahi kushiriki mashindano ya mbio nchini Japan. Jemeli, 26, anajivunia kutwaa ubingwa wa Prague Marathon katika nchi ya Jamhuri ya Czech kwa saa 2:21:57 mnamo Mei 7, 2017. Aliimarisha muda wake bora hadi saa 2:20:53 alipomaliza Berlin Marathon katika nafasi ya tatu mnamo Septemba 24, 2017.

Takriban wakimbiaji 20,000 wakiwemo wakali kutoka Japan na Ethiopia, wanatarajiwa kushiriki Nagoya Marathon mwaka 2018 .