Wakenya kujua rais mpya

Wakenya kujua rais mpya

NA BENSON MATHEKA

WAKENYA watajua rais wao mpya wakati wowote kuanzia sasa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati akiwa ana kesho Jumanne pekee kama siku anayopaswa kutangaza mshindi wa kura ya urais iliyofanyika Agosti 9, 2022.

Kulingana na Katiba, Bw Chebukati ambaye ni msamizi wa uchaguzi wa urais, ana siku saba tangu tarehe ya uchaguzi, kutangaza matokeo ya kura ya urais, siku ambazo zinakamilika kesho Jumanne.

Ibara ya 138(10) ya katiba ya Kenya inasema kwamba tume ya uchaguzi ina siku saba kutoka tarehe ya uchaguzi kutangaza mshindi wa kura ya urais.

“Ndani ya siku saba baada ya uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka aya (a) kutangaza matokeo ya uchaguzi; na (b) kuwasilisha ilani ya maandishi ya matokeo kwa Jaji Mkuu na rais aliye mamlakani,” inaeleza ibara hiyo.

Uchaguzi mkuu ulifanyika Agosti 9, 2022 na vituo vingi vilifungwa kabla ya saa kumi na moja jioni siku hiyo huku vichache vikichelewa kufungwa kwa kuwa vilifunguliwa kuchelewa.

Ujumuishaji na uthibitishaji wa matokeo kutoka maeneo-bunge yote 290 umekuwa ukiendelea kwa mwendo wa kobe katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi huku maafisa wa IEBC wakikagua na kutathmini fomu 34A kutoka katika zaidi ya vituo 46,000 vya kupigia kura kote nchini.

Mchakato huu umechukua muda mrefu huku Bw Chebukati akiwataka Wakenya kuwa na subira.

Hata hivyo, kulingana na katiba, mchakato huo ni lazima ukamilike kufikia leo Jumatatu usiku wa manane na mshindi kutangazwa ili kuepusha nchi dhidi ya mzozo wa kikatiba.

“Katiba iko wazi kuhusiana na suala hili. Mshindi wa urais lazima atangazwe siku saba kuanzia siku ya uchaguzi na kukosa kufanya hivyo kunaweza kutumbukiza nchi katika mgogoro wa kikatiba,” asema mtaalamu wa masuala ya uchaguzi Bw Tom Maosa.

Tofauti na chaguzi za awali, IEBC inakagua fomu zote 34A ili kuhakikisha zinawiana na 34B ambazo zinajumuisha matokeo ya urais kutoka vituo vyote vya kupigia kura katika kiwango cha eneobunge.

Bw Chebukati anasema ni lazima fomu zote za 34A kutoka vituo vyote vya kupigia kura zifikishwe kwake ili zikaguliwe na matokeo kuthibitishwa.

Bw Chebukati alisema kwamba IEBC imechukua kati ya saa tatu na saa nne kushughulikia afisa mmoja wa uchaguzi kutoka eneobunge moja.

“Kutokana na mchakato kuendeshwa pole pole, baadhi ya maafisa wa uchaguzi wamekuwa hapa kwa siku tatu, jambo ambalo halikubaliki,” Bw Chebukati alisema Jumamosi alipokuwa akielezea nchi hatua ambazo tume yake imechukua kuthibitisha matokeo ya kura ya urais.

Joto limekuwa likipanda katika ukumbi wa Bomas, washirika wa wagombeaji wakuu wa urais, Naibu Rais William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya wakishukiana na kurushiana lawama.

Bw Chebukati na makamishna wa IEBC walisema kwamba tabia ya washirika wa wagombeaji hao imekuwa ikichelewesha kazi ya maafisa wa IEBC ya kukagua na kuthibitisha matokeo.

  • Tags

You can share this post!

BI TAIFA AGOSTI 15, 2022

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu stadi, mbunifu kazini

T L