HabariSiasa

Wakenya kulipa mamilioni kurembesha makazi ya Ruto

May 23rd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA watatumia Sh152.4 milioni kufadhili ukarabati wa boma la pili la Naibu Rais Dkt William Ruto  jijini Mombasa, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Afisi ya Naibu Rais Novemba 2018 ilitangaza azimio la kupata mwanakandarasi kutengeneza boma la awali la kamishna wa mkoa kuwa boma la Naibu Rais.

Hazina ya Fedha itatenga Sh37.4 milioni kuanzia Julai mwaka huu ili boma hilo lirembeshwe. Boma hilo limo karibu na Ikulu ya Mombasa.

Zaidi ya Sh39 milioni zilizotengwa kwa ujenzi huo katika mwaka wa kifedha unaokamilika Juni, bajeti ya boma hilo kwa miaka miwili kabla ya uchaguzi wa 2022 ni Sh76 milioni, ambapo kiwango cha jumla kitakuwa ni Sh152.4 milioni.

Jumba hilo linatarajiwa kujengwa ili kufikia kiwango cha naibu wa rais. Kwa sasa, jumba hilo halina wakazi.

Aliyekuwa kamishna wa Mkoa wa Pwani na mratibu wa awali wa Pwani Samuel Kilele ndiye alikuwa wa mwisho kutumia jumba hilo.

Pia, wananchi watalipa mabilioni kujenga afisi ya pili ya naibu wa rais mjini Mombasa. Serikali ilikataa kumkodishia afisi Mombasa kutokana na hofu ya kiusalama, na badala yake kuamua kumjengea afisi.

Lakini mjini Nairobi, Naibu wa Rais William Ruto huishi nyumbani kwake, badala ya ikulu ya naibu wa rais Karen.