Habari za Kitaifa

Wakenya kupata afueni zaidi matatu zikipanga kushusha bei  

April 15th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

UONGOZI wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu Nchini (MOA) umedokeza kuwa unashauriana na wanachama wao kwa lengo la kupunguza nauli kwa kiwango cha hadi asilimia 10.

Mwenyekiti wa muungano huo Albert Karakacha Jumatatu, Aprili 15, 2024, alinukuliwa akisema kuwa kupunguzwa huko kwa nauli ni njia ya kutoa afueni wa Wakenya kufuatia hatua ya serikali kushusha bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa.

“Tumewasiliana na wanachama wetu katika maeneo ya Nairobi, Mombasa, Magharibi, Rift Valley na Kati mwa Kenya kuhusu haja ya kupunguzwa kwa nauli kwa asilimia 10. Baada ya kujenga maafikiano, tutatoa tangazo rasmi kupunguza suala hili hivi karibuni,” Bw Karakacha akaeleza.

“Tunatambua kuwa bila abiria biashara yetu haiwezi kunawiri. Hii ndio maana tumewaomba wanachama wetu kukubali wazo la kupunguza nauli hadi kiwango cha asilimia 10,” akaongeza.

Bw Karakacha alisema baada ya viongozi wa matawi yote ya MOA kukubaliana kuhusu kupunguzwa kwa nauli, viongozi hao hao ndio watahakikisha kuwa hatua hiyo inatekelezwa katika maeneo yao.

Alipendekeza kuwa kando na serikali kupunguza bei ya mafuta, inapasa kupiga hatua zaidi na kuhakikisha kuwa bei za vipuri na magurudumu ya magari pia zinapunguzwa.

Jumapili, Aprili 14, 2024, Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) ilipunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa kiwango kikubwa zaidi tangu Januari mwaka huu, 2024.

Bei ya petroli ilipunguzwa kwa Sh5.31 kwa lita moja, dizeli ikashuka kwa Sh10 huku bei ya mafuta taa ikiteremka kwa Sh18.68.

Hii ina maana kuwa jijini Nairobi na maeneo ya karibu lita moja ya dizeli itauzwa kwa Sh193.84, dizeli itauzwa kwa Sh180.38 na mafuta taa itauzwa kwa Sh170.06 kwa lita moja.

Bei za kuanzia Machi 14, 2024 hadi Aprili 14, 2025 ilikuwa Sh199.15 kwa petroli, Sh190.38 kwa dizeli na Sh188.74 kwa mafuta taa.

Bei hizo mpya zilianza kutekelezwa saa sita za usiku wa Aprili 14, 2024 hadi saa sita za usiku Mei 14, 2024.