Habari

Wakenya kupokea kadi za Huduma Namba

October 21st, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA huenda wakaanza kupewa kadi za Huduma Namba kuanzia Novemba baada ya kungojea kwa zaidi ya miezi 18.

Rais Uhuru Kenyatta alisema Jumanne kuwa kadi hizo zimetengenezwa na sasa serikali inasubiri Bunge kumuidhinisha Bi Immaculate Kasait aliyeteuliwa awe Kamishna wa Data, kabla ya kuanza kuzisambaza.

“Leo mmeshuhudia nimepokea kadi yangu. Sasa tunangojea bunge kumaliza kazi yake ya kupiga msasa kamishna wa data ili Wakenya kote nchini wapewe kadi zao mara moja,” akasema Rais Kenyatta.

Jumanne, Waziri wa Mashauri ya Ndani , Dkt Fred Matiang’i, alikabidhi Wakenya 12, akiwemo Rais Kenyatta na mkewe, Margaret, mwigo wa kadi za Huduma Namba.

Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza wakati wa sherehe ya Siku ya Mashujaa zilizoadhimishwa kitaifa katika Uwanja wa Gusii, Kaunti ya Kisii, aliwataka wabunge kuidhinisha Bi Kassait haraka ili kuwezesha serikali kusambaza kadi za Huduma Namba kwa Wakenya.

Iwapo ataidhinishwa, Bi Kassait ambaye ni mkurugenzi katika Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), atasimamia taarifa za kibinafsi zilizochukuliwa wakati wa usajili wa Huduma Namba.

Rais Kenyatta wiki iliyopita, alimteua Bi Kassait kuwa Kamishna wa Data kwa mujibu wa kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Kulinda Taarifa za Kibinafsi.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi wiki iliyopita aliitaka Kamati ya Mawasiliano na Ubunifu kumpiga msasa Bi Kassait na kuwasilisha ripoti yake bungeni ndani ya siku 14.

Wabunge, hata hivyo, wako likizoni na wanatarajiwa kurejea Novemba 3, mwaka huu.

Wabunge wa kamati hiyo huenda wakakatiza likizo yao ili kumpiga msasa Bi Kassait au wanaweza kuomba muda uongezwe.

Rais Kenyatta, wiki iliyopita, alilazimika kuzima joto baada ya wandani wa Naibu wa Rais kudai kuwa serikali inalenga kutumia Huduma Namba kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza katika chuo cha mafunzo ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (KWS) cha Manyani, kaunti ya Taita Taveta, pia alikanusha madai kuwa raia wa Ujerumani wamepewa kandarasi ya kutengeneza mfumo wa Huduma Namba.