Makala

Wakenya kutazama Tanzania ikihangaika huko AFCON kupitia KBC bila malipo

January 13th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAKENYA waliokuwa wametamauka kuhusu watakakofuatilia taifa la Tanzania likishiriki mitanange ya dimba la Taifa Bora barani Afrika (Afcon 2023) sasa wamepumua baada ya runinga ya kitaifa (KBC) kutangaza itapeperusha mitanange hiyo moja kwa moja.

Dimba hilo linaloandaliwa nchini Ivory Coast kati ya Januari 13 hadi Februari 11, 2024 lilikuwa limeingiza wasiwasi wa kukosa kupeperushwa hapa nchini baada ya Multichoice, wamiliki wa DSTV kutangaza New World TV inayomiliki haki za upeperushaji ilikuwa imekataa mkataba na runinga za hapa nchini.

Hata hivyo, waziri wa Michezo Ababu Namwamba alitangaza Ijumaa, Januari 12, 2024 kwamba “KBC imepata hatimiliki za kupeperusha mitanange hiyo moja kwa moja na kwa sasa kazi ni kwako kufuatilia”.

Kaimu Mkurugenzi wa KBC Bw Paul Macharia alisema kwamba mashabiki sasa watakuwa na uwezo wa kufuatilia dimba hilo pasipo ada zozote.

Kando na runinga ya KBC, shirika hilo la umma litapeperusha matangazo hayo kupitia idhaa 14 za redio na pia katika mitabendi za runinga ya Y254.

Dimba hilo la awamu ya 34 likishirikisha mechi 52 litahusisha timu 24, eneo la Afrika Mashariki likiwasilishwa na Taifa Stars ya Tanzania.

Tanzania iko katika kundi la F pamoja na Morocco, DR Congo na Zambia na mashabiki wengi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wanangojea kuona kama taifa hilo litafinywa au lifinyane katika awamu ya makundi hadi fainali.

Timu hiyo ya Tanzania chini ya ukufunzi wa Adel Amrouche inatamaniwa kwamba iwapo itakosa nafasi ya kwanza ambayo itatuzwa Sh1 bilioni za Kenya, basi iibuke ya pili ndio ituzwe kitita cha Sh630 milioni.

Kando na Tanzania, mataifa mengine katika dimba hilo ni wenyeji Ivory Coast, Nigeria, Equatorial Guinea, na Guinea-Bissau katika kundi A huku kundi B likijumuisha Misiri, Ghana, Cape Verde na Mozambique.

Kundi la C liko na Senegal, Cameroon, Guinea na Gambia huku kundi D likiwaleta pamoja Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola huku kundi E likiwa na Tunisia, Mali, Afrika Kusini na Namibia.

Mechi hizo zitaandaliwa katika nyuga za jiji kuu Abidjan, ndizo Felix Houphouet-Boigny na Alassane Ouattara Stadium.

Hizo zingine ni Yamoussoukro, Bouake, Korhogo na San Pedro.

Kwa sasa, kombe hilo liko na taifa la Senegal. Taifa la Misri ndilo limeshinda kombe hilo kwa mara nyingi zaidi ikiwa ni saba, Cameroon ikifuata kwa mara tano, Ghana mara nne na DRC na Ivory Coast mara mbili kila mmoja.

[email protected]