Habari za Kitaifa

Wakenya kuumia bei za gesi ya kupikia zikianza kupanda tena

February 14th, 2024 2 min read

BRIAN AMBANI Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wataanza kuumia tena, baada ya bei ya gesi ya kupikia kuongezeka.

Hali hiyo imetajwa kuchangiwa na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni.

Ni hali inayotarajiwa kuendelea kuwaongezea Wakenya mzigo wa gharama ya juu ya maisha.

Kwa mwaka mmoja uliopita, bei ya gesi ya kupikia imeongezeka kwa asilimia 1.7 nchini, hali ambayo pia imeshuhudiwa katika sehemu nyingine duniani.

Ongezeko hilo ni licha ya serikali kutangaza kukata ushuru uliokuwa ukitozwa gesi mwaka uliopita.

Mtungi wa kilo 13 ulikuwa ukijazwa kwa Sh3, 032 mnamo Desemba 2023, kulingana na takwimu kutoka kwa Halmashauri ya Kukusanya Takwimu Kenya (KNBS).

Bei hiyo ni ongezeko la Sh52, kwani mnamo Desemba 2022, kiwango sawa cha gesi kilikuwa kikijazwa kwa Sh2,980.

Hilo linamaanisha kuwa bei za gesi ya kupikia zimerejea katika kiwango zilikokuwa, kabla ya serikali kuiondolea ushuru.

Serikali ilitangaza kuondoa asilimia 16 ya kodi ya nyongeza (VAT) kwa gesi, ili kupunguza bei zake.

Kutokana na hilo, bei ya bidhaa hiyo ilipungua kutoka Sh3,069 Juni 2023, hadi Sh2,787 hapo Julai, hali iliyowafurahisha Wakenya wengi.

Hata hivyo, afueni hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani bei hizo zilianza kuongezeka tena, kwa kurejea pale pale zilipokuwa kabla ya ushuru huo kuondolewa.

Mwaka uliopita, thamani ya shilingi ya Kenya ilishuka sana dhidi ya dola ya Marekani, hali iliyoifanya iwe ghali kuagiza bidhaa kama gesi ya kupikia na mafuta.

Hilo ndilo lilichangia bei ya bidhaa hiyo kuongezeka ilipowasili nchini, hatua iliyorejesha nyuma mafanikio yaliyokuwa yamepatikana kwa kuondoa ushuru.

Katika miezi ya hivi karibuni, bei za bidhaa hiyo katika sehemu nyingine duniani pia zimekuwa zikipanda.

Wadadisi wanataja hilo kama pigo kwa serikali, kwani imekuwa ikitekeleza mpango wa kuongeza matumizi ya gesi miongoni mwa raia, kama sehemu za kushinikiza ukumbatiaji wa kawi safi.

Wakenya waliozungumza na Taifa Leo mnamo Jumanne waliirai serikali kuwalinda dhidi ya kuongezeka kwa bei hizo.

“Tumefika mwisho! Ni wakati serikali ituokoe sasa,” akasema Bi Mary Mwikali, ambaye ni mkazi wa eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.