Wakenya kuumia zaidi bei ya mafuta kipanda tena

Wakenya kuumia zaidi bei ya mafuta kipanda tena

Na HILLARY KIMUYU

WAMILIKI wa magari ya uchukuzi wa umma na ya kibinafsi watagharimika zaidi baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Bei ya Kawi na Petroli (EPRA) kuongeza bei ya mafuta kuanzia Ijumaa.

Kwenye taarifa, EPRA ilisema kuwa bei ya petroli ya supa, dizeli na mafuta taa itaongezeka kwa senti 17, Sh4.57 na Sh3.56 mtawalia kwa kila lita.

Hii inamaanisha kwamba waliowekeza katika sekta ya uchukuzi pamoja na Wakenya wengi wanaotumia mafuta taa watagharimika zaidi kununua mafuta kwa bei mpya hadi Februari 14.

Hapo awali, bei ya petroli ya supa ilikuwa Sh106.82, dizeli Sh91.82 na mafuta taa Sh83.56 kwa Wakenya wanaoishi jijini Nairobi.

“Mabadiliko hayo yanatokana na kupanda kwa bei ya kuagiza na kusafirisha mafuta ghafi. Gharama ya kuagiza petroli ya supa imepanda kwa asilimia 1.5 kutoka kwa Sh35,042 kwa kila lita mnamo Novemba, 2020 hadi Sh35, 571 mnamo Disemba 2020,” ikasema taarifa ya EPRA.

Kutokana na mabadiliko hayo, petroli ya supa sasa itauzwa Sh104.60 mjini Mombasa. dizeli itauzwa kwa Sh94.01 huku Mafuta taa ikiwa Sh87.08 mjini humo.

Katika mji wa Nakuru, petroli ya supa, dizeli na mafuta taa zote zitauzwa Sh106.69, Sh96.31 and Sh87.08 mtawalia. Mjini Eldoret, petroli itauzwa Sh107.61 huku dizeli na mafuta taa zikiuzwa Sh97.23 na Sh88 mtawalia.

Mjini Kisumu, petroli itauzwa Sh107.61, dizeli Sh97.23 na mafuta taa Sh87.99 mtawalia.Bei hizo zinajumuishwa ushuru wa VAT unaotozwa bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi kulingana na kifungu kwenye sheria za fedha nchini.

You can share this post!

Joto la siasa lapanda Pwani Ruto na Raila...

Mshindi wa urais Uganda kujulikana kesho