Habari

Wakenya kuumia zaidi Kenya Power ikipania kuongeza bei ya stima wakati huu wa janga la corona

November 5th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

GHARAMA ya maisha inatarajiwa kupanda nchini kufuatia mpango wa kampuni ya usambazaji umeme, Kenya Power, wa kutaka kuongeza bei ya kawi hiyo.

Duru kutoka mamlaka ya kusimamia sekta ya kawi nchini (EPRA) zinasema imeidhinisha ombi la kampuni hiyo la kutaka kuongeza bei ya umeme kwa hadi kiwango cha asilimia 20.

Inakisiwa kuwa hiyo ni sehemu ya mpango wa Kenya Power wa kujinasua kutokana na changamoto za kifedha, kiasi kwamba kampuni hiyo inazongwa na mzigo wa bei wa kununua umeme kutoka kwa wazalishaji kawi hiyo.

Ikiwa nyongeza hiyo itatekelezwa, ada za umeme zitaongeza mzigo kwa familia ambazo zinazongwa na mzigo wa kiuchumi unaotokana na janga la Covid-19.

Watengenezaji bidhaa na wafanyabiashara wengine pia watabebeshwa mzigo wa nyongeza ya gharama ya uzalishaji.

Hata hivyo, kabla ya nyongeza hii kutekelezwa lakini pendekezo hilo liwasilishwe kwa wananchi ili watoe michango, maoni na mapendekezo yao.

Kampuni ya Kenya Power ilikuwa imewasilisha ombi la kutaka bei ya umeme mnamo 2019 ambapo tume ya EPRA ilikubali pendekezo hilo. Hata hivyo, utekelezaji wa ombi hilo ulisitishwa kwa muda kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Ikiwa itapitishwa, nyongeza hiyo itachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali. Maelezo kamili ya nyongeza yatafichuliwa hivi karibuni.

Lakini kufuatia nyongeza hizo wateja wanaotumia umeme wa kiasi cha kilowati 100 kila mwezi watalipa Sh12.50 kwa kila kipimo kutoka ada ya sasa ya Sh10 kwa kila kipimo.

Wale watakaotumia zaidi ya kilowati 100 nao watalipa Sh19.53 kwa kipimo kimoja kutoka bili ya sasa ya Sh15.80 endapo nyongeza hiyo itapitishwa na EPRA.

Pendekezo hilo la nyongeza ya umeme linajiri wakati ambapo wananchi wanazongwa na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Covid-19.