Habari Mseto

Wakenya milioni 14.7 ni walalahoi – Ripoti

August 13th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyo na watu wengi zaidi walio maskini

Ripoti iliyotolewa na World Poverty Clock ilionyesha kuwa Kenya ni ya nane ulimwenguni miongoni mwa mataifa yaliyo na watu wengi zaidi walio maskini sana.

Barani Afrika, Kenya imeorodheshwa ya sita. Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 29 ya Wakenya (milioni 14.7) kati ya wananchi 49,684,304 ni maskini. Watu hao wanaishi chini ya Sh200 kwa siku (Sh5, 910 kwa mwezi).

Kutokana na hilo, huenda Kenya isiweze kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuhusiana na kupunguza viwango vya umaskini ulimwenguni ifikapo 2030.

Kulingana na ripoti hiyo, kaunti ya Turkana ina watu wengi zaidi wanaoishi chini ya kiwango kilichowekwa cha umaskini.

Asilimia 87.4(watu 756,306) katika kaunti ya Turkana. Inafuatwa na Bungoma ambayo ina asilimia 33.4 ya watu walio maskini zaidi (726,012) kati ya watu milioni 2.2.

Kaunti zingine zilizo na watu wengi maskini zaidi ni Wajir (asilimia 76), Narok (asilimia 49), Kwale (asilimia 41.3), Kilifi (asilimia 39.1), na Busia (asilimia 33.5).