Wakenya njaa viongozi wakipiga domo

Wakenya njaa viongozi wakipiga domo

NA MWANDISHI WETU

HALI sio hali tena kwa mamilioni ya Wakenya wa kawaida kutokana na usimamizi mbaya wa uchumi chini ya utawala wa Jubilee, ambapo sasa kila raia, kuanzia mtoto ambaye anazaliwa dakika hii, anadaiwa Sh137,000 kama deni la kitaifa.

Maisha yanapoendelea kuwa magumu kwa raia na uchumi kuzorota, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wamefumbia macho matatizo ya Wakenya, na badala yake kuelekeza nguvu zao kwenye siasa za BBI na uchaguzi mkuu wa 2022.

Wawili hao wanaopasa kutoa mwelekeo kwa taifa, wamesababisha migawanyiko ya kitabaka na kikabila kwa kukosa kuelewana kuhusu mwelekeo wa kitaifa, na sasa wanatumia muda wao mwingi kupiga siasa.

Naye Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye kama kinara wa upinzani wajibu wake ni kukosoa serikali wakati kama huu, amepoteza mwelekeo wa majukumu yake kwa kugeuka mtetezi sugu wa serikali .

Hii imetokea ikifichuka kuwa Serikali inakopa Sh2 bilioni kila siku, wiki mbili baada ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa kiasi sawa na hicho cha Sh2 bilioni kinaibwa katika serikali yake kila siku.

Usimamizi huu mbaya wa uchumi umefanya madeni ya Kenya kufikia Sh7.2 trilioni, ambapo kati ya pesa hizo, Sh5.3 trilioni zimekopwa tangu 2013 wakati Rais Kenyatta na Dkt Ruto walipoingia madarakani.

Hali hii mbaya ya uchumi imefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu kutokana na nyongeza ya kila mara ya ushuru serikali ikikazana kupata pesa za kulipa madeni na matumizi yake. Jambo ambalo limeongeza bei za bidhaa muhimu.

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) nayo imekuwa ikikimbizana na wafanyibiashara ambao tayari biashara zao zinaporomoka, pesa ambazo kulingana na rais wiki mbili zilizopita zinaishia kuibwa badala ya kutumika kwa miradi ya maendeleo.

Biashara zinapoendelea kufungwa, mamilioni ya vijana hawana namna ya kupata ajira, wakulima wanapunjwa na mabroka na hali ya kupoteza matumaini inaenea kote nchini.

Mishahara ya watumishi wa umma pia imeanza kucheleweshwa kutokana na uhaba wa pesa kwa serikali, mgao kwa kaunti unachelewa hadi miezi mitatu na hivyo kulemaza huduma muhimu kama afya, huku wafanyibiashara wanaoidai serikali na zile za kaunti wakifilisika na mali yao kupigwa mnada kwa kukosa kulipwa.

UFISADI

Hii ni hata baada ya Rais Kenyatta mara kwa mara kuagiza wizara na kaunti kuwalipa wafanyibiashara wanaozidai.

Kizungumkuti cha ukopaji wa serikali ya Jubilee ni mahala mikopo hiyo imeishia ikizingatiwa miradi mingi ya serikali huwa inakumbwa na ufisadi wa hali ya juu pamoja na rushwa.

Kinaya ni kuwa serikali inapanga kutumia mabilioni ya pesa kuandaa kura ya maamuzi kuhusu BBI wakati wanafunzi kutoka mazingira yenye umaskini wanasomea chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa miongoni mwa mahitaji mengine.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta aliwaahidi madiwani kote nchini Sh2 milioni kila mmoja za kununua magari.

Kulingana na Kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua, hatua hiyo ni sawa na kuwahonga ili wapitishe mswada wa BBI ambao unasubiri kujadiliwa na mabunge ya kaunti.

“Hii ni hongo kwa ajili ya kuwashawishi kupitisha mswada wa BBI,” akasema Bi Karua.

Katika kutonesha kidonda cha matatizo ya Wakenya, kwa kila Sh100 ambazo serikali inakusanya kama ushuru, Sh60 zinatumika kulipia madeni ya kigeni na ya humu nchini.

Cha kutamausha zaidi ni kuwa serikali inapanga kukopa zaidi, hali ambayo itaongeza deni la sasa la Kenya maradufu kufikia 2030.

Hali hii ya sasa ilipokuwa ikidorora, serikali iliendelea kupuuza ushauri wa taasisi kadhaa ikiwemo Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, ambayo ilikuwa ikihimiza serikali kupunguza kasi ya kukopa.

Mashirika mengine yaliyokuwa yakitahadharisha kuhusu hatari ya madeni ni Tasisi ya Wahasibu (ICPAK) na Taasisi ya Uchumi pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.

You can share this post!

KRU yasema vikosi viko tayari kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup

Mambo yalivyokuwa katika dirisha la uhamisho kwa Wakenya...