Wakenya nje ya vita vya medali ya soka ya viziwi Afrika

Na AGNES MAKHANDIA

WENYEJI Kenya wamebanduliwa katika mbio za kuwania medali kwenye soka ya mashindano ya Afrika ya Viziwi baada ya kulimwa 4-2 na Mali ugani Nyayo, Jumatano.

Kichapo hiki kilikuwa cha pili kwa vijana wa kocha Ben Omukuba baada ya kulemewa 3-1 na Senegal katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A ugani Kasarani mnamo Septemba 11.Kenya imetupwa katika mechi za kuorodheshwa nje ya mduara wa medali.

Omukuba alilaumu vijana wake kwa kutokaba wapinzani vyema, kukosa uzoefu na pia kutomanika.“Mbinu zetu pia zilikuwa mbovu. Tulikuwa na kasi nzuri tukifanya mashambulizi, lakini tulipoteza nafasi chungu nzima ovyoovyo.

Hata hivyo, soka huwa hivyo. Vijana wangali wadogo na wana maisha mazuri uwanjani siku za usoni,” alisema Omukuba.Mali ilitawala mchuano huo kwa nguvu za kimwili na pia kiufundi, huku kipa Diamane Camara akinyima wenyeji nafasi kadhaa murwa.

Mamadou Coulibally alifungua ukurasa wa mabao dakika ya kwanza. Nousa Keita aliimarisha uongozi huo dakika ya 37 alipokamilisha krosi ya Coulibally kupitia kichwa chake.

Kenya ilirejesha goli moja mapema katika kipindi cha pili kupitia penalti ya Bashir Yahye dakika ya 47 baada ya Kennedy Kiptoo kuangushwa kisandukuni.Yahye alisawazisha 2-2 kupitia penalti nyingine dakika ya 56 alipochezewa visivyo ndani ya kisanduku.

Hata hivyo, ufufuo wa Kenya haukudumu kwani Mali iliamka kutoka usingizini na kuchukua uongozi kupitia Seydou Cillouma dakika ya 71. Coulibally aligonga msumari wa mwisho dakika ya 76 alipomwaga kipa Mkenya Thor Mwai.