NA MWANGI NDIRANGU
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewarai Wakenya kupuuzilia mbali wito wa muungano wa Azimio la Umoja kwamba Jumatatu itakuwa siku ya mapumziko.
Badala yake, Bw Gachagua amewarai kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila hofu yoyote.
Bw Gachagua amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kuwa vikosi vya usalama vitakuwa katika hali ya tahadhari kukabili vitendo vyovyote vya ukiukaji wa sheria kutoka kwa waandamanaji.
“Hakuna lolote lipya kuhusu maandamano yanayoitishwa na baadhi ya watu. Ni suala ambalo tumeshuhudia kwa miaka mingi na hatutatishika kuwaruhusu watu wachache wabinafsi kujiunga na serikali kwa kutumia mlango wa nyuma,” akasema Bw Gachagua, akimaanisha kuwa mrengo wa Kenya Kwanza hautakubali wito wa handisheki.
Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, na viongozi wengine wanaoegemea mrengo wa Azimio wametangaza maandamano jijini Nairobi hapo kesho kulalamikia gharama kubwa ya maisha miongoni mwa masuala mengine. Bw Odinga ametangaza Jumatatu kuwa siku ya mapumziko ili kuwapa nafasi wafuasi wake kushiriki katika maandamano hayo kikamilifu.
Hata hivyo, Bw Gachagua, aliyekuwa akihutubu Ijumaa jioni katika Mkahawa wa Fairmont Mt Kenya Safari Club-Nanyuki, alitaja maandamano hayo kama wingu linalopita. Alikuwa akihutubu kwenye hafla ya kuwatuza wanahabari iliyoandaliwa na shirika la bima la Pan-African Re/Insurance.
“Watu hawa wamekuwa wakitoa jumbe za kuiogofya serikali iliyochaguliwa baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu. Tawala zilizopita zimekuwa zikikubali vitisho vyao kwa kuhofia uchumi kuvurugika. Hata hivyo, serikali ya Kenya Kwanza haitakubali vitisho hivyo,” akasema Naibu Rais.
Alitaja miito hiyo kama ukosefu wa uzalendo miongoni mwa viongozi wa Azimio, kwani wanazua hofu wakati uchumi wa Kenya umeanza kuimarika.
Alisema serikali ya Rais William Ruto imejitolea kuboresha maisha ya Wakenya kwa kuwavutia wawekezaji.
“Sekta ya bima huwa muhimu sana katika kukuza uchumi katika nchi yoyote ile. Wawekezaji huweza kujenga majengo mengi zaidi wakati majengo yaliyopo yanawekewa bima. Tunafaa kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kwa kubuni mazingira mazuri ya kufanyia biashara,” akasema.