Habari

Wakenya sasa wamlilia Okiya Omtatah awakomboe, wamfadhili kupitia M-Pesa

September 25th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah ambaye amegeuka mtetezi mkuu wa Wakenya kwenye masuala ya umuhimu wa kitaifa amezidi kupokea mkono wa msaada wa Wakenya ili kuzidi kufadhili kuwapigania mahakamani, wakati huu msukumo ukiwa kesi ya kupinga kutekelezwa kwa Sheria ya Ushuru 2018.

Hadi Jumanne, mwanaharakati huyo alikuwa amechangiwa Sh370,000 kupitia njia ya simu za kumpa motisha kuendeleza vita hivyo vya manufaa kwa taifa zima.

Tayari Bw Omtatah amewasilisha kesi kortini akipinga kutekelezwa kwa sheria hiyo ya kupandisha ushuru kwenye bidhaa za mafuta iliyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Katika kesi hiyo, Bw Omtatah anautaja ushuru huo kuwa kinyume na sheria na usiofaa, akisema kuwekwa kwa ushuru huo kunakiuka kifungu cha 47 cha katiba.

Aidha, Bw Omtatah ameeleza korti kuwa ushuru huo umeadhiri kwa njia mbaya bidhaa za kawaida na gharama ya maisha.

Lakini mwanaharakati huyo alieleza Taifa Leo Dijitali kuwa bado hana mpango wa kutumia pesa hizo, hadi atakapofanya mashauriano zaidi, akisema kila senti atakayotumia kutoka kwa pesa hizo itatumika ipasavyo.

“Sikua mmoja wa walioomba pesa hizi na hivyo siwezikuzichukulia kama ni zangu kibinafsi. Nitazifungia M-Shwari na kusubiri kufanya mashauriano ili nihakikishe nimezitumia kwa njia bora,” Bw Omtatah akasema.

Mchango huo ulianza baada ya mtumizi wa Facebook kuwaomba Wakenya wote wanaofanya kazi kumtumia Bw Omtatah Sh10, ili kumwezesha kuwapigania wananchi.

Mtumizi huyo alisema mchango huo utakuwa kama njia ya ‘kumrudishia mkono’ Bw Omtatah na pia za kuchapisha karatasi za kufanya kazi yake, na nauli.

“Kila Mkenya anayefanya kazi anafaa kumtumia kwa M-Pesa Bw Omtatah Sh10 za kutoa nakala za stakabadhi, chakula na nauli. Zinafaa kutimu Sh240 milioni,” akasema Kaka Baba.

Mchango huo unatumwa kwenye nambari 0722684777, kwa njia ya M-Pesa.