Wakenya Twitter wakerwa na kimya cha Raila bei ya mafuta ikipanda

Wakenya Twitter wakerwa na kimya cha Raila bei ya mafuta ikipanda

NA WANGU KANURI

WAKENYA katika mtandao wa kijamii wa Twitter wameshangazwa na kimya cha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wakati ambapo raia wanaumia na kulalamikia ongezeko la bei ya mafuta nchini.

Ongezeko hilo la bei ya mafuta lilitangazwa mapema wiki hii ambapo bei ya petroli kwenye jijini Nairobi ilipanda kutoka Sh 134.72 hadi Sh 127.14, bei ya dizeli ikawa Sh 115.60 kutoka Sh 107.66 nayo bei ya mafuta taa ikiongezeka kutoka Sh 97.85 hadi Sh 110.82.

Licha ya ongezeko hilo kuwa kero kwa wenye magari ya umma, Wakenya kwa jumla wanalalamika kila uchao na kuomba serikali iweze kuingilia kati na kupunguza bei hii ambayo itaathiri pakubwa namna zao za kujichumia riziki.

Ukimya wa kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga umezikereketa nyoyo za Wakenya wengi ambao wameonyesha hisia zao kupitia mitandao ya kijamii.

“Raila alikuwa ameipaza sauti yake wakati wa sakata ya fedha iliyoangaziwa ya NYS, Arror na Kimwarer, lakini sasa amenyamaza tena kuhusiana na ongezeko la bei ya petroli ambayo inamwathiri mwananchi wa kawaida kikamilifu. Anapaswa kuzungumza kuhusiana na ongezeko hilo ili afufue upya imani ambayo tulikuwa nayo,” akaandika Ja Loka kwenye Twitter.

“Raila amekuwa mnyamavu kuhusiana na masuala yanayoathiri Wakenya. Ukosefu wa ajira, ongezeko la juu la bei ya mafuta, majanga yanayoathiri sekta za Afya na Elimu, ufisadi, mapuuza ya katiba na haki za kibinadamu. Kwa makini sana anajitenga na chochote kitakachomuudhi Rais Uhuru na wenzake,” akaandika Timothy Mutua.

“Wanasiasa huzungumzia tu mambo ambayo yanawadhuru. Raila hawezi taka kumuudhi Uhuru na wenzake na ameamua kunyamaza sababu mtu haukati mkono unaompa chakula lakini tena yule hasla wa Karen amesema ama akafanya nini kuhusiana na suala hili?” akauliza @namelokLLB.

“Raila ni mtu muhimu sana kwenye serikali. Mnataka aseme nini ilhali yeye ni mmoja wa wanaotoa uamuzi nchini?” akauliza @EricohMaxwell.

“Raila Odinga husimamia tumbo lake peke yake,” akasema @Nick_andwem.

“Raila hapo kwenye upinzani kwa sasa. Kwa hivyo kudhibiti kinachofanywa na serikali si kazi yake,” akaandika @Nahashawn.

You can share this post!

Wito wawaniaji urais wenye ‘matumaini makubwa’...

Kuongeza bei ya mafuta kunaongezea umaskini Kenya –...