Michezo

Wakenya waambulia pakavu kwenye tuzo za kimataifa za Wanariadha Bora wa Mwaka 2020

December 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MONDO Duplantis wa Uswidi na Yulimar Rojas wa Venezuela walitawazwa Wanariadha Bora wa Mwaka 2020 na Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia mnamo Disemba 5, 2020.

Kenya iliambulia pakavu kwenye tuzo hizo zilizoshuhudia washindi wakitangazwa kupitia mtandaoni.

Licha ya kuibuka bingwa wa Nusu Marathon ya Dunia na kuvunja rekodi ya mbio za nusu marathon mara mbili, Mkenya Peres Jepchirchir alibwagwa na Rojas aliyevunja rekodi mbili za fani ya kuruka mbali mara tatu (long jump) mwaka huu.

Jepchirchir alivunja rekodi ya nusu marathon ya dunia kwa mbio za wanawake pekee mnamo Septemba 5, 2020 alipokamilisha kivumbi cha Prague Half Marathon kwa muda wa saa 1:05:34. Baadaye, mwanariadha huyo alivunja rekodi yake hiyo alipokamilisha mbio za Nusu Marathon ya Dunia kwa muda wa saa 1:05:16 mnamo Oktoba 17, 2020 nchini Poland.

Jepchirchir na Rojas walikuwa miongoni mwa wanariadha watano waliounga orodha fupi ya mwisho kati ya 10 walioteuliwa kuwania tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.

Wawaniaji wengine wa tuzo hiyo walikuwa Letesenbet Gidey (Ethiopia), Elaine Thompson-Herah (Jamaica) na Sifan Hassan (Uholanzi).

Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) pia liliambulia patupu kwenye kitengo kipya cha kuwania tuzo ya Shirikisho Bora la Mwaka mwanachama wa WA. Shirikisho la Riadha la Poland lilitawazwa mshindi wa kategoria hiyo.

Licha ya janga la corona kuvuruga kalenda ya mashindano mbalimbali ya riadha mwaka huu, Shirikisho la Riadha la Poland lilifanikiwa kuandaa mapambano ya haiba kubwa yakiwemo matatu ya Riadha za Dunia za Mabara (World Athletics Continetal Tour). Mawili kati ya mashindano hayo yalifanyika mjini Chorzow huku jingine likiandaliwa jijini Bydgoszcz.

Kwa pamoja na kamati ya kitaifa ya riadha, Shirikisho la Riadha la Poland lilifaulu pia kuandaa mbio za Nusu Marathon ya Dunia mnamo Oktoba 17 jijini Gdynia.

Kwa upande wake, Kenya ilifanikiwa kuandaa makala ya Kip Keino Classic mnamo Oktoba 3, 2020. Makala hayo yalikuwa ya mwisho kwenye kalenda ya mbio za Dunia za Mabara mnamo 2020.

Mbali na Kenya na Poland, wawaniaji wengine wa tuzo hiyo mpya miongoni mwa mashirikisho bora ya riadha walikuwa Peru, Palestine, Nicaragua na New Zealand.

Duplantis ambaye hakushindwa katika mapambano yote 16 aliyoshiriki katika mwaka wa 2020, alivunja rekodi ya dunia katika fani ya kuruka juu kwa ufito (pole vault) mara mbili kwa mita 6.17 kisha mita 6.18. Isitoshe, aliweka rekodi ya mita 6.15 kwenye mashindano ya ukumbini.

Duplantis alimpiku pia Joshua Cheptegei wa Uganda aliyepigiwa upatu wa kutwaa taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanaume. Cheptegei alivunja rekodi tatu za dunia katika mbio za mita 5,000 (dakika 12:35.36), mita 10,000 (dakika 26:11.00) na kilomita tano barabarani (dakika 12:51). Mtimkaji huyo aliambulia nafasi ya nne kwenye Nusu Marathon ya Dunia nchini Poland licha ya kwamba alikuwa akishiriki mbio hizo kwa mara ya kwanza.

Kilele cha ufanisi wa Duplantis katika fani ya michezo mwaka huu ni ushindi wa wazazi wake Greg na Helana waliotwaa tuzo mpya ya makocha bora wa mwaka almaarufu Coaching Achievement Award.

Picha ya watoto waliokuwa wakishiriki mbio za nyika za Discovery Cross Country Championships mjini Eldoret mnamo Januari 2020 ilitwaa tuzo ya Picha Bora ya Mwaka. Picha hiyo ilipigwa na Michael Steele ambaye ni raia wa Uingereza.