Habari Mseto

Wakenya waandamana Amerika kupinga serikali kuhangaisha upinzani

February 13th, 2018 2 min read

Na CHRIS WAMALWA na RICHARD MUNGUTI

KIKUNDI kikubwa cha Wakenya wanaoishi Amerika kiliandamana Jumamosi nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa kupinga dhuluma za serikali dhidi ya viongozi wa upinzani nchini na wanahabari.

Waandamanaji hao ambao wengi ni wafuasi wa Muungano wa NASA wanaoishi katika eneo la Tri-State lililoko New York, Connecticut, New Jersey na Pennsylvania walivumilia mvua kubwa, upepo na baridi.

Walibeba mabango na kusoma taarifa za malalamishi ambazo baadaye ziliwasilishwa kwa maafisa wa UN.

“Tunataka jamii ya kimataifa ijue kuhusu matukio yanayoendelea nchini Kenya ambapo ukiukaji wa sheria na ukosefu wa heshima kwa mahakama, uhuru wa vyombo vya habari na sheria unachukuliwa kama jambo la kawaida. Jamii ya kimataifa hasa mataifa ya magharibi hayafai kunyamazia ukiukaji huu,” akasema Bi Beatrice Oduor, kwenye taarifa yake.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, ilikosolewa na wengi waliozungumza katika maandamano hayo wakisema matukio yanayoshuhudiwa ni ufufuzi wa kukandamiza wakosoaji wa serikali jinsi ilivyokuwa katika utawala wa kiimla wa rais mstaafu Daniel arap Moi.

 

Ukiukaji wa haki

Kulingana nao, tukio la kufurushwa kwa Bw Miguna Miguna nchini halikutokea ghafla bali ni mambo ambayo yamekuwa yakiendelea kutokana na ukiukaji wa haki za uchaguzi, ufisadi, ukiukaji wa sheria na ukwepaji wa sheria.

Wakati huo huo, mawakili wa Miguna wameishtaki Serikali wakiomba akubaliwe kurudi nchini bila vikwazo, arudishiwe pasi na kutosumbuliwa tena.

“Wakenya walijitahidi sana kujiondolea kutoka minyororo hiyo. Makovu ya enzi hizo bado yanaonekana kitaifa ndiposa tumeamua kwa pamoja kwamba hatutaruhusu tena udikteta urejee Kenya,” akasema Bw Nick Ogutu, wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International, tawi la Amerika.

Walisema serikali ambayo haina hatia na iliyo halali haiwezi kuchukua hatua kama hizo dhidi ya wananchi wake isipokuwa iwe inajishuku.

“Afisi ya rais ndiyo imekuwa mkiukaji mkubwa zaidi wa sheria za taifa. Ikiwa uvunjaji wa sheria unaendelea kuwa jambo la kawaida, kutakuwa na machafuko,” akasema Bw Jackton Ambuka, kutoka Neww Jersey.

Maandamano hayo yaliandaliwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ya Amnesty International (Amerika), Kenya Yetu Initiative na Muungano wa Wakenya walio Ughaibuni Amerika.