Habari Mseto

Wakenya wachangisha Sh1.2 milioni kwa matibabu ya mtoto India


MTOTO wa miezi 11 anayehitaji upasuaji muhimu ili kuokoa maisha yake Jumapili, Juni 16, 2024 alilazwa katika hospitali ya Fortis Memorial nchini India baada ya Wakenya kuchangisha Sh1.2 milioni.

Haya yamejiri baada ya Taifa Leo kuchapisha kuhusu kisa cha mtoto huyo kwa jina Arianna Wairimu, Alhamisi iliyopita, Juni 13.

Bi Teresa Ndung’u, alifichua kuwa sehemu kubwa ya waliochanga walitoa Sh100 na Sh200, na kumpa matumaini mtoto huyo ya kupata matibabu maalum anayohitaji.

“Ni Mungu tu na mimi tunaojua jinsi nilivyojawa na shukran. Wimbi la matumaini ambayo msaada huo umeeneza kwa familia na mtoto wangu ni la kipekee,” Bi Ndung’u alieleza Taifa Leo.

Kuhusu bili ya Sh6 milioni inayohitajika kwa upasuaji huo, Bi Ndung’u alisema “sasa tumebakisha Sh2 milioni.”

Juhudi za awali za kumwokoa mtoto huyo ambaye madaktari walimpa hadi Julai 5, 2024 kama mwisho wake kuwa hai kama asingelifanyiwa upasuaji huo, ziliwezesha kuchangisha Sh3 milioni.

Bi Ndung’u amekuwa akiishi hospitalini tangu aliposafiri kutoka nyumbani kwake Kaunti ya Nyandarua, Mei 17, 2024, ili kuwasihi madaktari kutoka India kumhudumia mtoto wake huku akitafuta pesa.

Huku wingu jipya la matumaini likitanda, Bi Ndung’u anasema matumaini yake yote ni kwa msaada “mamilioni yanayotajwa sijawahi kamwe hata kuyaota.”

Ili kutuma mchango unaweza kutumia Nambari ya Paybill: 522533, Akaunti 7834867 (Hazina ya Matibabu ya Mtoto Arianna) Nambari ya Mpesa: +254 720 677064.