HabariSiasa

Wakenya wachemka kupinga ada ya ujenzi wa nyumba

April 18th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA Jumatano walionyesha ghadhabu kubwa kuhusiana na mpango wa serikali kuwatoza ada ya Mpango wa Kitaifa wa Ujenzi Nyumba, huku mahakama ikisimamisha utekelezaji wake.

Jumatano, Mahakama ya Uajiri na Masuala ya Leba jijini Nairobi ilisimamisha utekelezaji huo, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanunuzi Bidhaa Kenya (COFEK).

Serikali inapanga kuwatoza watu walioajiriwa asilimia 1.5 katika mishahara yao kama ada ya mpango huo.

Jaji Maureen Onyango alitoa agizo hilo, akisema kuwa kusimamishwa kwake kutatoa nafasi ya kuunganishwa kwa kesi zilizowasilishwa na COFEK na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU).

Ikiongozwa na Katibu Mkuu wake Stephen Mutoro, COFEK inashikilia kuwa utekelezaji wa mpango huo utawaongezea Wakenya mzigo wa ushuru mkubwa wanaotozwa na serikali.

“Si haki kuwashinikiza wananchi kuchangia mpango wa nyumba ambazo huenda zisiwafaidi baadaye,” kikasema kwenye malalamishi yake.

Kupitia wakili Henry Kurauka, COFEK pia ilisema kuwa si Wakenya wote walioweka umiliki wa nyumba kama suala muhimu kwao, hivyo hawapaswi kulazimishwa kuuchangia.

Walimu vile vile walipinga mpango huo, wakiutaja kama njama ya serikali kuendelea kuwapunja wananchi.

Kiongozi wa Chama cha Amani (ANC) Musalia Mudavadi pia alipinga mpango huo akisema, kuwa Wakenya wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

“Kutokana na hali ngumu ya maisha na kiangazi kinachoendelea, haifai hata kidogo kumwongezea mwananchi mzigo mwingine wa ushuru,” akasema Bw Mudavadi kwenye kikao na waandishi, jijini Nairobi jana.

Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KUPPET) kiliilaumu serikali kwa kutangaza kuanza kuutekeleza mpango huo, licha ya kesi iliyo mahakamani.

“Tumeshangazwa sana na mpango wa serikali kuanza kututoza ushuru huu, licha ya pingamizi nyingi zinazouhusu ambazo zimetolewa,” akasema Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Moses Nturima.

Mahakama ya Masuala ya Leba ilikuwa imesimamisha utekelezaji wake hadi Mei 20, ambapo kesi ingeanza kusikizwa kikamilifu.

Bw Nturima alisema kuwa chama hicho kitatumia njia zote kiwezavyo kuhakikisha hautekelezwi kama ulivyo.

Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) nacho kilisema kuwa walimu hawatakubali kutozwa ushuru huo hadi pale serikali itawaongeza zaidi ya asilimia tisa ya mishahara yao.

Mnamo Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waajiri Kenya (FKE) Jacqueline Mugo aliwaomba kutotekeleza mpango huo, kama walivyoagizwa na Wizara ya Ujenzi na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA).

“Tunawaomba kutotekeleza agizo lililochapishwa na Wizara ya Ujenzi na KRA katika vyombo vya habari kwani hauna msingi wa kisheria. Tutawaarifu kuhusu hatua mtakazochukua,” akasema kwenye taarifa.Kwenye mitandao ya kijamii, Wakenya wengi vile vile walieleza ghadhabu zao, wakishikilia kuwa mpango huo unapaswa kuwa wa hiari.

Katika mtandao wa Twitter, wengi waliupinga kupitia mjadala #PingeniUshuruwaNyumba.

“Baadhi ya Wakenya tayari wanamiliki nyumba. Mbona wachangie mpango mwingine kama huo?” akashangaa Henry Makori. Serikali imeshikilia kuwa ni lazima iutekeleze, kwani unawiana na lengo la Rais Uhuru Kenyatta kusuluhisha tatizo la umiliki nyumba nchini kupitia Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Wakenya wengi pia wameonekana kutoukumbatia, kwani kufikia jana, ni Wakenya 210,319 pekee waliokuwa wametuma maombi ya kupata nyumba kupitia tovuti: bomayangu.co.ke.

Serikali inalenga kujenga nyumba 500,000 za bei rahisi kufikia 2022.