Dimba

Wakenya wachemkia timu ya ndondi Hit Squad kwa kukosa kufuzu kwa Olimpiki

June 4th, 2024 3 min read

NA CHARLES ONGADI

BAADA ya Kenya kushindwa kufuzu Michezo ya Olimpiki katika mashindano ya ndondi ya dunia jijini Bangkok, Thailand, wiki iliyopita wadau wa masumbwi nchini wametofautiana kuhusu matokeo hayo.

Juhudi za mabondia wote sita wa Kenya kufuzu Olimpiki na kuzima ukame wa miaka 36 tangu taifa lishinde medali katika michezo hiyo, zilitumbukia nyongo wakilambishwa sakafu nchini Thailand wiki jana.

Kulingana na msemaji wa Shirikisho la Ndondi Kenya (BFK), Duncan ‘Sugar Ray’ Kuria, kushindwa kwa mabondia wa Kenya ni kutokana na mfumo mbaya wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na maandalizi duni ya timu ya taifa.

“Ni jambo la kuhuzinisha hatukupata mwakilishi katika Olimpiki kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu. Vijana walijaribu, lakini hawakufaulu,” akasema Kuria.

Alieleza kuwa mfumo mpya uliotumiwa na IOC, wa kutaka kuleta usawa wa kijinsia katika Olimpiki kwa kupunguza idadi ya washiriki, ulichangia mno kuzima ndoto ya Kenya.

Kuria alifichua kwamba kinyume na mfumo wa awali uliotumiwa na Chama cha Kimataifa cha Ndondi (IBA), ambapo mshindi wa kwanza hadi wa tatu alipata tiketi ya moja kwa moja, IOC inatoa nafasi moja pekee katika kila uzani.

Vile vile, kuandaa ndondi za kufuzu katika kila bara kuliipa Kenya nafasi finyu kutwaa tiketi ya Olimpiki, tofauti na miaka ya nyuma ambapo kila nchi ilipata nafasi pasipo kupitia mchujo.

Msemaji huyo wa BFK pia alikiri maandalizi ya timu ya taifa, maarufu Hit Squad, yalikuwa duni ikilinganishwa na wapinzani wao walioshirikishwa mapigano mengi ya kimataifa ya kujipima nguvu kabla kutua Bangkok kwa mashindano hayo ya kufuzu.

Ni kauli inayoendelezwa na bondia wa zamani wa klabu ya KPA, Bernard Kilongozi, aliyedai kuwa pia uteuzi mbaya wa timu ya taifa umechangia katika matokeo mabovu.

Ubaguzi katika uteuzi wa kikosi

Kilongozi alisema kumekuwa na ubaguzi mkubwa katika uteuzi Hit Squad ambapo mabondia kutoka sehemu moja pekee ndio hutwikwa jukumu la kupeperusha bendera ya taifa bila kuzingatia uwezo wao wa kutamba kimataifa.

“Kama uteuzi wa timu ya taifa utafanywa kwa njia ya haki na usawa kama miaka ya nyuma, basi Kenya itarudi tena katika ramani ya mchezo huu Afrika na duniani,” alieleza katika mahojiano na Taifa Spoti.

Alitoa mfano wa bingwa wa miaka miwili wa Ligi Kuu na mashindano mengine, Mwinyi Faki wa Mombasa, ambaye amepuuzwa kikosini.

Lakini mwenyekiti wa kamati ya kiufundi ya BFK, Albert Matitob, akitofautiana na madai hayo ya ubaguzi alisema kilichoramba Hit Squad ni kukosa uzoefu wa kushiriki mapigano ya kujipima nguvu kimataifa.

“ Mabondia wetu walipambana vizuri ila walikosa uzoefu na maandalizi kabambe ya kushiriki mashindano makali,” akasema kocha huyu wa zamani wa klabu ya jeshi (KDF) akiwa Kisumu.

Vile vile, Matito alihoji kwamba wakati umewadia kwa BFK kualika wataalamu wa kimataifa katika benchi ya kiufundi ya Hit Squad ili kusaidiana na makocha walioko wa humu nchini kuimarisha ujuzi wao.

Kenya ilikuwa taifa la kwanza bara Afrika kushinda medali ya dhahabu katika Olimpiki; mwaka 1988 kupitia Robert Wangila jijini Seoul, Korea Kusini naye Mkenya mwenzake Chris Sande akanyanyua shaba.

Hata hivyo, juhudi za mabondia wake kufuzu Olimpiki zilisambaratika hata baada ya kunogesha Mashindano ya Afrika jijini Accra, Ghana, mwaka jana kisha yale ya dunia nchini Italia kabla kumalizia Thailand wiki jana.

Uzito wa Bantam

Amina Martha Faki katika uzito wa Bantam, Friza Anyango wa Welter na Elizabeth Andiego wa Middle wote walipoteza mapigano yao katika mzunguko wa kwanza.

Kwa upande wa wanaume Boniface Mogunde wa Lightmiddle na Peter Abuti wa Heavy walibanduliwa katika mzunguko wa kwanza, kabla Edwin Okong’o wa Lightheavy kushindwa katika mzunguko wa pili.

Kenya itakosa mwakilishi wa ndondi katika Olimpiki kwa mara ya kwanza kwa miongo minne. Tangu michezo hiyo kuanza 1964, timu ya taifa imekosa makala ya 1974 jijini Montreal, Canada na ya 1974 jijini Moscow, Urusi.

Naye Samson Yakoub Mtoni alihoji kwamba mashindano ya zamani kama Brunner/Urafiki yaliyoshirikisha nchi za Afrika Mashariki yanafaa kufufuliwa ili kuwaweka mabondia katika hali nzuri kila wakati.

“Zamani timu ya taifa ilifana kutokana kwamba mabondia wetu walishiriki mashindano mengi ya nje kujinoa, ambayo yaliwapiga msasa kwa mashindano makubwa kama ya Dunia,” akasema Mtoni ambaye pia ni kocha wa zamani wa timu ya taifa.