Makala

Wakenya wachongoana mitandaoni wakisherehekea ‘April Fool’s Day’

April 1st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KILA mwaka, Wakenya huungana na dunia nzima kusherehekea Siku ya Kupumbazana (April Fool’s Day), ambayo huadhimishwa Aprili mosi.

Kulingana na wanahistoria, siku hiyo haina asili maalum, ingawa wengi wao husema ilianza kusherehekewa karne nyingi zilizopita.

Mwaka huu, hali haikuwa tofauti, kwani Wakenya wengi waliweka jumbe za kukanganya jamaa na marafiki wao wa karibu, ambao hawakuwa wamebaini kwamba siku hii huwa ya kupotoshana—yaani kutoelezana ukweli.

Katika mitandao ya kijamii, Wakenya maarufu na wenye ufuasi mkubwa waliweka jumbe ambazo ziliwaacha mashabiki wao wakiwa wamejaa maswali kuhusu ukweli wa yale waliyoyasema.

Miongoni mwa ‘macelebs’ waliozua mihadalo ni wanahabari Larry Madowo na Kamene Goro.

Madowo alizua hisia miongoni mwa mashabiki wake, baada ya kusema kuwa ameacha kazi katika shirika la habari la CNN nchini Amerika, na kujiunga na kituo cha BBC, alikokuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na CNN.

“Kwa mashabiki wangu, ningetaka kuwafahamisha kwamba nimeacha kazi katika shirika la CNN na kujiunga na shirika la BBC, jijini Washington, Amerika,” akasema, kwemye mtandao wa X (zamani ukijulikana kama Twitter).

Ingawa baadhi ya mashabiki wake walionekana kukubali ujumbe huo, kuna wale walioeleza taswishi zao.

Mary Wakesho alisema kuwa tangu utotoni, babake alikuwa akisikiliza shirika la habari la BBC, likipeperusha matangazo yake kutoka jijini London, Uingereza.

“Kwani shirika hilo limebadilisha makao yake? Nadhani unatupotosha kimakusudi,” akasema Bi Wakesho, hali iliyoonekana kuwafungua macho mashabiki wengine wa mwanahabari huyo, kwamba hii ni Siku ya Kupumbazana.

Mwanahabari Kamene Goro naye aliwaacha mashabiki wake wakiwa na hisia mseto, baada ya kusema kuwa amerejea kwenye kituo kimoja cha redio alikokuwa akifanya kazi kama Afisa Mkuu Mtendaji, wala si mtangzaji!

Ni ujumbe ulioonekana kuthibitishwa na kituo hicho.

“Tunamkaribisha Kamene Goro tena kama afisa mkuu mtendaji!” Kikaeleza kituo hicho, kwenye ujumbe kilichoweka Instagram.

Licha ya siku hiyo, mizaha hiyo kuonekana kuendelezwa na Wakenya wengi wanaotumia mitandao ya kijamii, na wale walio katika maeneo ya mijini, wakazi wengi katika maeneo ya mashambani waliendelea na shughuli zao bila kutambua uwepo wa siku hiyo.

“Mizaha kama hiyo huwa inaendelezwa na vijana. Binafsi, siitambui siku hiyo. Niliamkia kazi yangu kutafutia familia yangu riziki kama kawaida,” akasema Bw Martin Wanjohi, ambaye ni mkazi wa mji wa Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.