Habari Mseto

Wakenya wachunguze vyama kabla ya kuwekeza fedha – EACC

March 26th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi(EACC), wamewataka Wakenya kuchunguza kwa makini kabla ya kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo, ili kuzuia kulaghaiwa fedha zao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak, alisema tatizo kubwa linalozonga vyama vingi vya ushirika ni uongozi usiofaa na ufisadi unaotekelezwa na wakuu wa vyama hivyo. Alisema wakuu hao wanaviunda ili kujiendeleza kwa pesa za wanachama.

“Inasikitisha Wakenya waliokuwa wamejawa na matumaini ya kufikia makubwa maishani kwa kuwekeza fedha zao katika vyama vya ushirika wanatapeliwa na kusalia bila chochote,” alisema Bw Mbarak.

Aliongeza, “Hata hivyo wanafaa kujilaumu wenyewe kwa kukimbilia utajiri wa haraka bila kuchunguza kwa makini jinsi vyama hivyo vinavyoendeshwa.”

Afisa huyo alikuwa akizungumza wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya EACC na vyama vya akiba na mikopo jijini Nairobi. Makubaliano hayo yatahakikisha kwamba EACC inahusika pakubwa kudhibiti masuala yanayoendelea ndani ya vyama hivyo. Bw Mbarak pia aliwataka wanachama wa vyama husika kuchukua tahadhari kabla ya kuwadhamini wanachama wenzao kuchukua mikopo baada ya kubainika wengi hutoroka kisha kuwaachia wadhamini mzigo mzito wa kulipa fedha zilizokopwa.

Ingawa hivyo, aliuhakikishia uongozi wa vyama vya akiba na mikopo kuwa watashirikiana nao kuwaandama wanaohepa kulipa mikopo yao.

Mwenyekiti wa EACC, Askofu Mstaafu Eliud Wabukala, naye alisifu mafanikio ambayo vyama vya ushirika vimesaidia wananchi wengi ila akaonya kwamba matukio ya ufisadi huenda yakayeyusha nia ya wengi kuwekeza kwa vyama hivyo.

“Binafsi vyama hivi vimenisaidia sana kufanya masuala mengi ya kibinafsi. Hata hivyo kama tume, ushirikiano huu utatuwezesha kuingilia kati na kurejesha uaminifu, nidhamu na maadili katika vyama vyetu,” akasema Bw Wabukala.

Kutiwa saini kwa makubaliano haya ya kudhibiti shughuli za vyama vya ushirika kunajiri baada ya wanachama wa Ekeza Sacco inayosimamiwa na Mhubiri mwanasiasa David Kariuki Gakuyo, kupoteza fedha zao baada ya kubainika walilaghaiwa.