Wakenya waendelea kuishinikiza IMF kukoma kuikopesha Kenya

Wakenya waendelea kuishinikiza IMF kukoma kuikopesha Kenya

Na SAMMY WAWERU

WAKENYA mitandaoni wameendeleza mchakato wa kulishinikiza Shirika la Fedha Duniani (IMF) kufuta mkopo wa Sh257 bilioni kwa serikali.

Chini ya alama ya reli #StoploaningKenya, wameelekeza hasira zao katika kurasa za mitandao ya IMF, wakisisitiza mkopo huo utayafanya maisha kuwa magumu zaidi hasa kipindi hiki taifa linaendelea kung’atwa na makali ya janga la Covid-19.

Serikali iliomba mkopo huo na ambao umeidhinishwa, ikihoji utasaidia kuimarisha kampeni dhidi ya virusi vya corona nchini.

Hata hivyo, Wakenya wameshikilia utaishia mifukoni mwa mafisadi. Katika kila chapisho la IMF mitandaoni, wanalivamia wakihimiza shirika hilo kufuta mkopo huo.

“Komeni kuwekelea kizazi kijacho mzigo mzito wa kulipa ushuru na mikopo mnayotoa kwa serikali ya Kenya. Uongozi serikalini ni kitovu cha ufisadi na ufujaji wa mali ya umma. Mjifunze na msaada wa Jack Ma na ambao uliibiwa mchana peupe, hautatufaidi #StoploaningKenya,” #Favoured Mburu Nganga akaandika kwenye mojawapo ya chapisho kwenye Facebook.

“IMF tunaomba msubiri hadi pale tutapata viongozi wenye uwazi. Hatuna budi ila kukita kambi katika machapisho yenu ili mtilie maanani kilio cha wanyonge wanaoendelea kukandamizwa, #StoploaningKenya,” Florence Kerry akachangia.

Billy Graham Kegode alilitaka shirika hilo kujua Wakenya wamechoshwa na visa vya ufisadi kugonga vichwa vya vyambo vya habari, akisema itakuwa busara IMF kufuta mkopo huo.

Katika ukurasa wa IMF Twitter, wembe ni ule ule. “#StoploaningKenya, mnafanya Wakenya milioni 54 kuwa watumwa,” @Emmanuel Mugambi akaandika.

“Hatutaki mikopo yenu, komeni kuipa serikali,” akasisitiza @STAN-LEE.

Hamaki za Wakenya zinaendelea kushuhudiwa mitandaoni, serikali ikianza msako kuzima wanaoikosoa Facebook na Twitter.

You can share this post!

Ufugaji wa kuku riziki tosha kwake

LEONARD ONYANGO: Ukweli ni kuwa Kenya yahitaji suluhu ya...