Habari

Wakenya wagonga ufalme wa Dubai

May 15th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MWANAMFALME wa Milki ya Kiarabu (UAE), Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, alitapeliwa Sh400 milioni na walaghai kutoka Kenya katika sakata ya dhahabu feki, ambapo Seneta Moses Wetangula wa Bungoma ametajwa.

Bw Wetangula amekanusha kwamba alihusika na sakata hiyo. Sakata hiyo iliendeshwa na matapeli ambao meneja wa kampuni inayomilikiwa na Sheikh Mohamed anasema walikuwa na ulinzi wa maafisa wa polisi.

Kulingana na maafisa wa Dubai, matapeli hao waliwasiliana na kampuni ya Zlivia inayomilikiwa na Sheikh Mohamed wakidai walikuwa na tani tano za dhahabu kutoka Ndande Tribe, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambayo walitaka kuuza.

Kulingana na stakabadhi ambazo meneja meneja wa kampuni ya dhahahabu kutoka Dubai, Ali Zandi, aliwasilisha kwa maafisa wa upelelezi, matapeli hao walidai kwamba dhahabu hiyo ilitwaliwa na kuzuiliwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta baada ya kusafirishwa kutoka DRC kwa barabara kupitia Uganda

Police wanasema kwamba sakata hiyo ilianza Septemba 25, 2018 matapeli walipowasiliana na Zandi, ambaye pia ni mpwa wa Sheikh Mohamed. Walimshawishi kwamba wangemuuzia tani 4.6 za dhahabu kutoka DRC na walihitaji pesa za kufanikisha shughuli hiyo.

Duru za polisi zinasema kwamba walaghai hao walitumia wafanyabiashara maarufu akiwemo raia mmoja wa Urusi ili kumshawishi Zandi kwamba walikuwa na dhahabu kutoka Congo ambayo wangeuza Dubai.

Baadaye walidai kwamba dhahabu hiyo ilikuwa imezuiwa na maafisa wa forodha katika uwanja wa JKIA na Bw Zandi akawasiliana na Bw Wetangula amsaidie ili iachiliwe na kusafirishwa hadi Dubai.

Kwa mwaliko wa Zandi, inasemekana Wetangula alisafiri hadi Dubai mnamo Desemba 15, 2018 ambapo aliwahakikishia kwamba angewasaidia dhahabu hiyo iachiliwe.

Kulingana na ripoti ya Zandi, alikataa kutoa Sh200 milioni anazodai Wetangula alimwitisha na akaamua kuja Kenya binafsi ambapo alijaribu kukutana na maafisa wa serikali lakini hakufaulu.

Akiwa Kenya, alipelekwa katika uwanja wa JKIA ambapo alionyeshwa makasha yaliyodaiwa kuwa na dhahabu. Ikizingatiwa kuwa JKIA huwa kwenye ulinzi mkali, iliibuka kuwa baadhi ya matapeli hao ni watu wenye ushawishi serikalini ambao huwapeleka raia wa kigeni maeneo yasiyoruhusiwa ambako huwa wanatumia kuendeleza biashara yao haramu.

Mnamo Januari 21 mwaka huu, Zandi anadai kwamba alikutana na mtu aliyedaiwa kuwa waziri serikalini.

Kulingana duru za polisi, alihakikishiwa kwamba dhahabu yake ingeachiliwa lakini hakuipata na wapelelezi wanasema hakukuwa na dhahabu katika makasha yaliyokuwa JKIA.

Sheikh Maktoum aliandikia Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i barua akitaka serikali ya Kenya iachilie dhahabu yake. Kwenye barua hiyo, Sheikh Mohamed anasema anafahamu shehena hiyo ilichelewesha kufuatia shambulizi la kigaidi katika hoteli ya Dusit2 mnamo Februari mwaka huu.

Bw Zandi anasema akiwa Nairobi alishauriwa akodishe ndege ya kampuni ya humu nchini kutoka uwanja wa Wilson ili kusafirisha dhahabu hiyo bila kutambuliwa. Anaeleza kwamba mnamo Januari 25 alifungwa macho na kupelekwa eneo fulani ambako alipata maafisa wa polisi na kufahamishwa kwa mwanasiasa maarufu.

Licha ya kukodisha ndege hakuruhusiwa kuingia eneo la kupakia mizigo katika uwanja wa JKIA. Kulingana na Zandi, alipompigia simu mtu aliyedai kuwa ni Dkt Matiang’i alimweleza kuwa ndege hiyo ilikuwa chini ya ulinzi wa maafisa maalumu kwa sababu kuna mtu aliyetaka kuiba dhahabu hiyo.

Mnamo Machi 7, Bw Zandi alilazimika kulipa Sh45 milioni za gharama ya ndege ambayo ilidaiwa kupakiwa katika JKIA.

Sakata hiyo ilipochapishwa katika magazeti ya humu nchini, anadai kwamba Wetangula alimshauri aondoke nchini kwa usalama wake na akalazimika kukodisha helikopta hadi Kisumu ambapo alikodisha ndege ya kibinafsi hadi Dubai.