Habari

Wakenya wagonjwa wakwama ughaibuni

April 14th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI Jumanne ilisema kuna maelfu ya Wakenya ambao wamekwama katika nchi mbalimbali za kigeni wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya maisha kufuatia masharti makali ya kupambana na virusi vya Corona ulimwenguni.

Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Bw Macharia Kamau, jana alisema miongoni mwa wale waliokwama ng’ambo ni wagonjwa waliosafiri kutafuta matibabu na jamaa walioandamana nao.

Wengine ni watalii, wanafunzi na Wakenya wengine ambao wako katika nchi za kigeni bila vibali.

Inaaminika wengi waliokwama katika nchi za kigeni wakitafuta matibabu kwa magonjwa mbalimbali, wako nchini India ambapo shughuli zote zilisitishwa kama njia ya kupambana na ueneaji virusi vya corona.

Akizungumza jana katika kikao cha wanahabari Nairobi, Bw Macharia alisema serikali ina wasiwasi kuhusu hali ya Wakenya walio India.

“Kuna zaidi ya Wakenya 64 ambao wamekwama India. Walikuwa wameenda kwa matibabu. Tunaamini kuna wengi zaidi. Wengine wao wameishiwa na pesa kwa sababu hawakutarajiwa kukaa huko kwa muda mrefu,” akasema.

Alifichua kuna wagonjwa wengine ambao kwa bahati mbaya walifariki, lakini hakuna jinsi jamaa zao wanaweza kusafirisha miili hadi nyumbani.

“Pengine huu ni wakati wetu kuamua kuruhusu wapendwa wetu azikwe mahali ambako watafariki,” akasema.

Bw Macharia alisema kufikia sasa, kuna Wakenya saba ambao wanashukiwa walifariki kwa kuambukizwa corona katika nchi za nje. Watano kati yao walifariki Amerika, na wawili nchini Sweden.

“Kuna Wakenya wengine kadhaa ambao bado ni wagonjwa. Wengine wao wamepona katika nchi mbalimbali,” akasema.

Kulingana na Bw Macharia, serikali kwa sasa haina uwezo wa kurudisha Wakenya walio ng’ambo nyumbani kwa kuwa kuna maagizo yaliyozuia safari za ndege katika nchi nyingi za nje.

Alisema afisi za ubalozi zinafanya kila juhudi kutafuta Wakenya wote walio katika mataifa ya kigeni ili kuwasaidia kwa kila njia iwezekanavyo.

Katibu huyo alisema kwamba, kufikia sasa, serikali imepokea ripoti za wanafunzi 21 waliokwama Hungary, huku watu wengine 61 wakikwama Ufaransa.

Katika mataifa ya Uarabuni, alisema inahofiwa kuna Wakenya wengi ambao wamepoteza kazi.

Idadi kubwa ya Wakenya ambao huenda kutafuta kazi katika mataifa ya Milki ya Kiarabu hufanya kazi za vibarua.

Barani Asia, alisema nchi inayofuatiliwa zaidi ni China na India.

“Kuna takriban Wakenya 3,000 China, na idadi ni kubwa zaidi kwa sababu tunajua kuna wengi ambao hawajasajiliwa katika ubalozi wetu. Hatujapokea kisa chochote cha raia wetu kufariki China,” akasema.

Alieleza kuwa Kenya inashirikiana na China kuhakikisha matukio yaliyoshuhudiwa jijini Guangzhou hivi majuzi, ambapo Wafrika waliteswa na maafisa wa serikali, hayatatokea tena.

Wakenya takriban 18 walikwama Australia walipoenda kutalii, na wanafunzi 200 wanasemekana kukwama Iran kwa kuwa masomo hayaendelei ilhali hawana uwezo wa kurejea nyumbani.

“Tumewasiliana na serikali zote kimataifa kuwaomba wasaidie Wakenya sawa na jinsi sisi tunavyosaidia raia wa kigeni ambao wanaishi humu nchini,” akasema.

Alisisitiza kwamba kwa sasa, ombi la viongozi na wananchi kuwa Wakenya wanaoteseka ng’ambo warudishwe nyumbani haliwezi kutekelezwa kwa sababu usafiri wa ndege umekwamishwa duniani kote.