Habari Mseto

Wakenya wahimizwa kuvalia mavazi yaliyoundwa nchini

December 4th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MWITO wa kuvalia mavazi yaliyoundiwa nchini Kenya unazidi kupigiwa chapuo huku kaunti kadha zikihimiza wakazi wake kuvalia nguo za kutoka Kenya.

Kaulimbiu ‘Jenga Kenya kwa Kununua Bidhaa za Kenya’ inashabikiwa tangu Oktoba 17, 2019, Rais Uhuru Kenyatta aliposema lengo kuu lilikuwa ni kuinua uchumi wa Kenya na kuzipiga jeki kampuni zinazounda nguo nchini.

Mojawapo ya kampuni zinazohimiza zaidi mwito huo ni Thika Cloth Mills ambayo mkurugenzi wake ni Tejal Dhodhia.

Miaka ya tisini (1990s) viwanda vya kushona nguo hapa nchini vilinawiri ajabu lakini baada ya nguo za mitumba kupenya hapa nchini, viwanda vilisambaratika na wafanyakazi wengi kupoteza kazi zao.

Baadhi ya viwanda vilivyofungwa ni Kenya Textile Mills ya Thika, Kikomi ya Kisumu na Rivatex ya Eldoret.

Hata hivyo, kampuni ya Thika Cloth Mills ilijikakamua na kubaki licha ya mawimbi hayo mazito hata ingawa ilibaki na wafanyakazi wachache.

Bi Dhodhia ambaye ndiye mkurugenzi wa kiwanda hicho anasema walipitia mambo mazito lakini waliweza kubaki katika ushindani mkubwa wa biashara.

“Licha ya kuwa na pandashuka tele za hapa na pale tulilazimika kuzuru maeneo mengi kama Pwani na maeneo ya Nyanza kwa minajili ya kutafuta pamba ambayo ndiyo tulikuwa tukitumia kwa wingi,” akasema mkurugenzi huyo.

Hata sekta za binafsi zimejitosa katika wito huo wa ‘kujenga Kenya na kununua Kenya’.

Mwito uliotolewa unahimiza wafanyakazi wawe wakivalia mavazi ya viwanda vya nchini hasa kila Ijumaa ili kutangaza umuhimu wa kuinua uchumi wa nchi.

Bi Dhodhia anatoa mwito wa kuhimiza kuvalia mavazi ya kuundiwa Kenya ili pia kuambatana na ajenda nne muhimu za serikali.

“Hivi majuzi tulipozuru kaunti nne muhimu kama Homa Bay, Kisumu, na Siaya tulipata ya kwamba wakazi wa maeneo hayo wamekubali kwa kauli moja kuwa wataanza kupanda mipamba kwa fujo ili kuhakikisha viwanda vilivyofungwa vinafunguliwa tena.

Hivi majuzi mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alipeleka mswada bungeni wa kuzuia bidhaa kutoka nje kuingizwa hapa nchini kwa vile baadhi yazo zinaundiwa hapa nchini.

Alisema iwapo nchi hizo zitakubaliwa kuingiza bidhaa zao hapa nao watozwe ushuru mara tano ya ule wa kawaida.

Mawaziri na madiwani (MCA) wa kutoka kaunti ya Kiambu tayari wamepogeza hatua hiyo ya mbunge huyo wakisema ni nia nzuri ya “kuinua uchumi wetu.”

Uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba nchi ya Kenya inaingiza bidhaa kutoka nje zifikazo thamani ya Sh2 trilioni kila mwaka, huku ikitumia Sh500 bilioni kwa bidhaa za kutoka nje. Inakadiriwa pia bidhaa za asilimia 25 zinatoka nchini China.