Habari Mseto

Wakenya wahofia njaa corona ikizidi

April 20th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya Wakenya wanahofia kuwa watakosa chakula na mahitaji mengine muhimu endapo janga la virusi vya corona litaendelea kwa miezi kadhaa.

Matokeo ya utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na shirika la Infotrak, asilimia 76 ya Wakenya wanahofia kuwa watakosa chakula janga la corona likidumu kwa miezi mitatu ijayo na zaidi.

Wakenya hao walisema kuwa hawana rasilimali za kutosha kuwawezesha kupata mahitaji muhimu janga la corona likiendelea kwa muda mrefu.

Wakazi wa Kaskazini Mashariki wanaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walio na hofu kuhusiana na janga la virusi vya corona kwa asilimia 82.

Asilimia 79 ya wakazi wa ukanda wa Bonde la Ufa walioshiriki katika utafiti huo walisema kuwa wana hofu kubwa kuhusiana na janga la corona, Nyanza (78), Kati (76), Mashariki (74), Magharibi (73), Nairobi (69) na Pwani (67).

Serikali tayari imeanza kutoa msaada wa fedha kwa familia zisizojiweza kimapato.

Wakenya pia wanatilia shaka uwezo wa hospitali za Kenya kuhudumia waathiriwa wa virusi vya corona endapo idadi kubwa yao itapatikana na viini hivyo.

Kwa mujibu wa Infotrak, asilimia 73 ya Wakenya wanahisi hospitali za Kenya hazina vitanda vya kutosha kulaza idadi kubwa ya wagonjwa wa virusi vya corona.

Hata hvyo, asilimia 55 wameridhishwa na mikakati iliyowekwa na serikali katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Kati ya Wakenya 831 waliohojiwa, asilimia 78 ya Wakenya wanaamini kuwa kuna maelfu ya watu wanaotembea na virusi vya corona mwilini bila wao kujua.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa ni asilimia 15 tu ya Wakenya ambao hawafuatilii habari kuhusu virusi vya corona kwa ukaribu.

Asilimia 82 wamekumbwa na hofu na msongo wa mawazo kuhusu janga la corona huku asilimia 55 wakihisi upweke.

Asilimia 38 ya waliohojiwa pia walisema kuwa habari kuhusu corona zinawashtua kiasi cha kukosa usingizi usiku.

Ni asilimia 8 tu ya Wakenya ambao hawana hofu ya kuishiwa na fedha endapo janga la corona litaendelea kwa miezi kadhaa.

Asilimia 61 ya Wakenya wanaamini kuwa wizara ya Afya inayoongozwa na Bw Mutahi Kagwe inafanya kazi nzuri.

Rais Uhuru Kenyatta anafuatia kwa asilimia 59, wahudumu wa afya (58) na vyombo vya habari vinafunga jedwali la nne bora kwa asilimia 52.

Bunge na polisi ni miongoni mwa idara ambazo Wakenya wanasema kuwa zimefanya machache katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Idadi kubwa ya Wakenya wanataka serikali iwape msaada Wakenya wasiojiweza kimapato.

Asilimia 23 wanataka serikali kuhakikisha kuwa hakuna Mkenya atapoteza ajira kufuatia janga la corona.