Habari Mseto

Wakenya wakerwa na Gavana Kimemia kutumia Sh12 milioni kununua Mti wa Krismasi

December 23rd, 2020 1 min read

NA WANGU KANURI

Gavana wa Kaunti ya Nyandarua Francis Kimemia ameshangaza Wakenya kutumia Sh12 milioni kununua Mti wa Krismasi huku wakazi wengi katika kaunti yake wakisalia maskini wasioweza kumudu bei ya machopochopo ya sikukuu.

Kupitia Wizara ya Kaunti ya Elimu, Utamaduni na Sanaa, gavana huyo aliwaalika wakazi wa mtaa wa Maironya katika uzinduzi wa mti huo Jumatano kuanzia saa tano asubuhi. Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa mti huo ulinunuliwa nchini Italia na kusafirishwa humu nchini.

Tangazo hilo liliibua hisia tata katika mtandao wa kijamii wa Twitter huku Wakenya wakionekana kukerwa na mazoea ya wanasiasa kupunja fedha za mlipa ushuru bila kujali.

“Hivi kuna pesa za kununua mti wa Krismasi wenye dhamana wa milioni 12 wakati ambapo barabara za kaunti ya Nyandarua hazipitiki. Ujasiri ulio na kaunti hii umekithiri mipaka, ” akaandika @Kianangih.

“Weee kwani huu Mti wa Krismasi una nini?” akauliza @The_Karanja.

“Wakati kuna janga, nchi inatatizika kupata ushuru, madaktari hawalipwi, shule hazina maski na unachukua milioni 12 na unanunua mti wa Krismasi na unapata ujasiri wa kuandika katika mitandao wa kijamii. Je tunaweza kuwa na sheria itakayotuwezesha kuwachoma wakuu wengine wa serikali?” akasema @OmetoBryson.

“Pesa zilikuwa zishaibiwa. Walikuwa wanatafuta kusawazisha hesabu za kaunti,” akaandika @kibuchi_g.

“Je madaktari wa kaunti hiyo wana vifaa vya kujikinga vya PPE? Je madaktari wao hao wamelipwa mishahara yao ya mwezi huu ama bado yamechelewa? Kivipi wakaazi wa Nyandarua watanufaika na mti huu?” akauliza @EMungau.

“Ninafikiri kuwa viongozi wa kaunti hiyo wameruka vichwa,” akasema @Robertkashu