Habari MsetoSiasa

Wakenya wakerwa na kimya cha wanasiasa vigogo

April 3rd, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KUTOSIKIKA kwa wanasiasa maarufu nchini tangu janga la virusi vya corona lilipoibuka, kumewakera Wakenya na kuibua maswali kuhusu kimya chao na hatua wanazochukua kuisaidia serikali kukabiliana na hali hiyo.

Miongoni mwao ni Naibu Rais William Ruto, kinara wa ODM Raila Odinga, kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Bw Moses Wetang’ula.

Ingawa Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, alisema kuwa ndiye pekee ambaye atakuwa akitoa taarifa kuhusu hali ya virusi hivyo nchini, kimya cha wanasiasa hao kimeibua taswira ambayo si ya kawaida miongoni mwa Wakenya wengi.

Baadhi yao hata hivyo, wamekuwa wakiweka picha katika mitandao ya kijamii wakiwa majumbani mwao au wakijumuika na familia zao.

Kwa kawaida, wanasiasa kama Dkt Ruto na Bw Odinga huwa wanatoa taarifa kuhusu watakakokuwa au misimamo mbalimbali ya kisiasa kupitia mitandao ya kijamii kama Twitter na Facebook. Hilo ndilo huwafanya Wakenya wengi kuwafuata kwenye mitandao hiyo.

Hata hivyo, hali ni tofauti mara hii, kwani kurasa zao hazina jumbe nyingi.

Kwa mfano, katika kurasa za Dkt Ruto, shughuli ya mwisho ya umma aliyohudhuria ni Maombi ya Kitaifa kuhusu Virus vya Corona yaliyofanyika kwenye Ikulu ya Nairobi mnamo Machi 21.

Taarifa aliyotoa ya mwisho kuhusu hali ya nchi ni kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ndingi Mwana a’Nzeki.

Hali ni vile vile kwa Bw Odinga, kwani sawa na Dkt Ruto, maombi hayo ndiyo yalikuwa hafla yake ya mwisho kuhudhuria.

Baadaye, Bw Odinga aliweka ujumbe kuwatahadharisha Wakenya kuzingatia maagizo wanayopewa na Wizara ya Afya kuhusu njia za kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Kulingana na Bw Mark Bichachi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda wanasiasa hao wamenyamaza kutokana na uzito wa maambukizi ya virusi hivyo.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ jana, Bw Bichachi alisema kwamba itakuwa nadra sana kwa mwanasiasa yeyote kutoa taarifa ya kisiasa wakati huu, kwani ataonekana kutojali hali ilivyo nchini na duniani kote.