Wakenya wakerwa na mbunge kuzindua televisheni

Wakenya wakerwa na mbunge kuzindua televisheni

Na MARY WANGARI

TUKIO ambapo Mbunge wa Kesses, Swarrup Mishra, alizindua televisheni katika sherehe ya kukata na shoka limevutia hisia mseto pamoja na kuwavunja mbavu Wakenya mitandaoni.

Kupitia picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii wikendi, mbunge huyo anayefahamika pia kwa jina la utani kama Arap Chelule, alionekana akiongoza uzinduzi huo katika kituo cha Cheplaskei Peace Centre, mjini Kesses.

Huku akimulikwa na kamera kadhaa, mtunga sheria huyo wa chama tawala cha Jubilee, alionekana akikata mapambo yenye rangi ya samawati na dhahabu yaliyofunga televisheni hiyo ya inchi sabini iliyoangikwa kwenye ukuta.

Kitendo hicho kiliibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya wengi wao wakionekana kukata tamaa na utendakazi wa viongozi wao. Kufuatia kisa hicho, wananchi walifurika katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook ambapo walieleza hisia zao.

“Ikiwa hawa ndio viongozi wetu, tumeisha…tumeisha kabisa,” alisema Khan“Na huenda hafla hiyo iligharimu mamilioni ya pesa. Inahuzunisha,” Stella Githaiga alilalamika.

“Mbunge wa Kesses azindua runinga kisha mnashangaa mbona tumeandamwa na masaibu tele kama taifa,” alifoka Soko Analyst.

“Jameni, ilhali tunazungumzia kuhusu ruwaza 2030, au tuseme Kesses ilihitaji hii zaidi kushinda barabara, huduma bora ya afya na mazingira tulivu ya kufanyia biashara. Wapiga kura wapendwa, mnastahili viongozi bora,” alisema Brian Wamukota.

“Naam, katika habari nyinginezo, Mbunge wa Kesses azindua televisheni,” alisema Mohamed Hersi.

You can share this post!

Wachuuzi 500 wakosa pa kuuzia baada ya vibanda kubomolewa...

Okutoyi aporomoka tena kwenye viwango bora vya tenisi...