Habari Mseto

Wakenya walazimika kutafuta matibabu Tanzania

January 20th, 2020 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

HUKU serikali ikinuia kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanapata huduma bora za afya kufikia mwaka wa 2022, wenyeji wa kaunti ya Taita Taveta wangali wakisafiri hadi Tanzania kutafuta matibabu.

Taifa Leo ilibaini kuwa idadi ya wenyeji wa eneo hilo wanaosafiri hadi Tanzania kutafuta matibabu imeongezeka.

Baadhi ya familia zimelazimika kupeleka wagonjwa wao katika hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) iliyo Moshi na Faraja iliyo Himo, baada ya hospitali za kaunti hiyo kukumbwa na uhaba wa vifaa na dawa.

Katika kijiji cha Bura Ndogo mjini Taveta, familia moja imeanzisha mbinu za kuchangisha fedha za matibabu ya mwana wao aliyelazwa katika hospitali ya KCMC, Tanzania.

Familia hiyo inahitaji Sh100 000 ili kumwezesha mtoto huyo wa miaka 14 kufanyiwa upasuaji wa haraka kuondoa uvimbe tumboni mwake.

“Tulienda katika hospitali mbalimbali za kaunti hii na mwisho wakatushauri tutafute matibabu kwingine,” akasema mjombake mwathiriwa, Bw Juma Miraj.

Mgonjwa mwingine, Bw Patrick Mnyange anauguza maumivu nyumbani siku mbili baada ya kuruhusiwa kuondoka katika hospitali ya Faraja, al maarufu Kwa Minja.

Mkewe Bi Floice Ruciana alisema kuwa mume wake alinusurika kifo baada ya kukatwakatwa kwa panga na kisha kukosa matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Taveta.

“Tuliamua kumkimbiza Kwa Minja kwa kuwa hatukupata matibabu hapa na vilevile hospitali haikuwa na dawa,”akasema.

Mbunge wa Taveta, Dkt Naomi Shaban alishtumu serikali ya kaunti inayoongozwa na Gavana Granton Samboja kwa kushindwa kuboresha sekta ya afya katika kaunti yake.