Habari Mseto

Wakenya waliteseka 2018, watarajia hali bora 2019

January 1st, 2019 2 min read

NA LILYS NJERU

JAPO mwaka uliopita wa 2018 ulikuwa na changomoto chungu nzima kwa wananchi, Wakenya wengi mwaka huu wa 2019 wameomba kila mmoja awe na utu na roho ya kusaidia wengine.

Ukosefu wa kazi, kufutwa kiholela na waajiri na kukosa kutimiza ahadi kwa wapendwa wao kutokana na gharama ya juu ya maisha ni baadhi tu za changamoto nyingi zilizowakosesha Wakenya usingizi mwaka 2018. Kulingana na Wycliffe Asuga, 32 ambaye ni baba wa mtoto mmoja, alishuhudia kwa masikitiko akiba yake yote ya Sh100,000 ikiisha vivi hivi asibakie hata na senti mwaka uliopita.

“Mwaka jana nilikuwa na lengo la kununua kipande cha ardhi ili nijenge nyumba yangu kwa kuwa familia yangu imekuwa ikiishi katika nyumba ya kukodisha. Nilianza kudunduiza fedha mwanzo wa mwaka huo ila kila kitu kilienda mrama baadaye,” akasema Bw Asuga.

Baba huyo na mkewe wanafanya kazi ya upigaji rangi viatu jijini Nairobi na kwa pamoja walilenga kutimiza ahadi hiyo ila katikati ya mwaka wa 2018 mambo yaliwaharabikia baada ya mkewe kukumbwa na maradhi.

“Katikati ya mwaka wa 2018, aliugua ghafla na hangeweza kuendelea na kazi yake. Akiba yangu yote iliishia kwenye gharama za matibabu. Kwa sasa anatarajiwa kufanyiwa oparesheni mwisho wa mwezi huu na nina wingu la matumaini oparesheni hiyo itafaulu,” akasema Bw Asuga.

Kilichotia msumari moto kwenye kidonda cha Bw Asuga hata hivyo ni jinsi idadi ya wakazi wa jijini wanaofika kwenye vibanda vyao vya upigaji rangi ili kuhudumiwa ilivyopungua pakubwa.

“Mimi ni maskini kwa sababu kile ninacholipwa sasa ni ya kujikimu tu. Hata hivyo mambo yakinyooka 2019, huenda nikaanzisha kilimo cha ufugaji katika kijiji changu mashinani, “ akaongeza Bw Asuga.

Masaibu yayo hayo pia yanamkumba Collins Ouma, 26 ambaye kwa sasa anatafuta ajira. Kwa wiki kadhaa Bw Ouma amekuwa akitembelea ofisi nyingi jijini Nairobi akiwa amejihami na vyeti vyake akiomba ajira ila bado hajafanikiwa.

Kulingana naye, mwaka wa 2018 ulikuwa mgumu sana. “Nilianza biashara ya kuuza nguo mwezi Juni ila ikaporomoka Agosti. Baadaye nilipata kandarasi ya kuwa mlinzi na kampuni moja ya usalama. Kwa sasa nasaka ajira kwa udi na uvumba,” akasema Bw Ouma. Vile vile kijana huyo anatia dua usiku na mchana ili aweze kupata fedha za karo ili arejee Chuo Kikuu cha Kenyatta kukamilisha shahada ya elimu aliyokuwa akisomea.

Wengine kama Peris Muthoni, afisa wa usalama hata hivyo alishabikia mno mwaka wa 2018 baada ya kufaulu kumsajili mwanawe kusomea Chuo Kikuu cha Nairobi. “Ingawa sikuweza kufikia malengo yangu ya kifedha niliyojiwekea, nafurahi sana kwamba niliweza kumsajili mwanangu chuoni ili aweze kusoma. Natumai mwaka wa 2019 utakuwa wa heri,” akasema Bi Muthoni. Kulingana na matokeo ya utafiti wa kampuni ya TIFA, asilimia 56 kati ya Wakenya 1,267 waliohojiwa walikemea sana mwaka wa 2018 wakiutaja kama mbovu zaidi.

Hii ilitokana na changamoto kama gharama za juu ya maisha, ukosefu wa ajira na umaskini.