Habari Mseto

Wakenya wamkaanga mamaye msichana mlevi mitandaoni

January 4th, 2019 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

WAKENYA Ijumaa walimkaanga mamaye mwanafunzi wa kike aliyeonekana amelewa chakari kwenye video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, wakisema wazazi wa siku hizi wamelemewa na majukumu yao ya ulezi.

Kwenye video hiyo iliyosambazwa kwenye Facebook, Twitter na Instagram, msichana huyo anaonekana ameshikwa na mama fulani huku akiropokwa kuwa alilewa kumuiga mama yake.

“Ninakunywa pombe kwa sababu mama yangu na shangazi yangu pia hulewa. Unafaa kufuata mfano wa mamako mzazi, ndio maana ninalewa,” alipayuka msichana huyo kwa lugha ya Sheng’.

Wapita njia wanasikika wakishangaa jinsi msichana huyo badala ya kwenda shule alikwenda kujiburudisha kwa baa.

Ilibainika kuwa msichana huyo ni mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Kangubiri Girls iliyoko Kaunti ya Nyeri, lakini tangu shule zifunguliwe hakuwa amefika shuleni kufikia jana.

Taifa Leo ilipomtembelea mwanafunzi huyo wa kidato cha pili nyumbani kwao eneo la Karatina, alifichua kuwa alinunuliwa pombe hiyo na rafiki yake katika mojawapo ya maduka, na kwamba hii ilikuwa mara yake ya kwanza kuonja vileo.

“Tulienda msalani katia hoteli moja ambapo tulikunywa pombe hiyo. Nilianza kujihisi nimelewa na sikujua kilichotokea baadaye,” akasema.

Hata hivyo, Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni dhidi ya Mihadarati (NACADA) iliahidi kumsaidia msichana huyo kujiepusha na vileo.

“Msichana huyu anafaa kusaidiwa badala ya kukejeliwa. Anahitaji makuzi ya maadili si kushindia kumkosoa,” akasema mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw Vincent Mutua.