Habari Mseto

Wakenya wammiminia sifa Kibaki akigonga umri wa miaka 89

November 16th, 2020 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Mstaafu Mwai Kibaki jana Jumapili alitimu umri wa miaka 89 huku Wakenya wakitumia mitandao ya kijamii kummiminia sifa tele na kumwombea maisha marefu.

Wakenya walimpongeza kwa juhudi zake katika kufufua uchumi, uliokuwa umeporomoka, mara alipochukua hatamu za uongozi Desemba 30, 2002.

Rais Kibaki aliyestaafu mnamo 2013 baada ya kukamilisha kipindi chake cha mihula miwili, anakumbukwa kwa kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa Barabara Kuu ya Thika.

Kibaki pia alianzisha elimu ya msingi bila malipo, hatua iliyoongeza idadi ya watoto waliokuwa wakijiunga na shule.

Mnamo Juni 10, 2008, Kibaki alizindua Ruwaza ya 2030 yenye nia ya kukweza Kenya kuwa miongoni mwa mataifa ya uchumi wa kati.

“Heri njema za siku ya kuzaliwa Mheshimiwa Kibaki. Ulizindua malengo ya maendeleo ya 2030 lakini mrithi wako Rais Uhuru Kenyatta akapuuzilia mbali,” akasema Irungu Nyakera kupitia mtandao wa Twitter.

“Kibaki alikuwa na nidhamu katika ukopaji wa fedha kutoka ughaibuni. Aliacha deni la Sh900 bilioni lakini Rais Kenyatta amekopa hadi Sh7 trilioni na ufisadi umekolea serikalini,” akasema Bw Evans Mwiti.

Baadhi ya Wakenya, hata hivyo, walikosoa rais huyo watatu wa Kenya kwa kuchangia katika ghasia za bada ya uchaguzi wa 2007 alipoapishwa usiku.