HabariSiasa

Wakenya wamponda 'Baba' kwa kuunga mkono ushuru wa 8%, wamwita msaliti

September 19th, 2018 2 min read

VIVERE NANDIEMO na PETER MBURU

WAKENYA wakiongozwa na Raila Odinga Junior wamemkashifu babake na kiongozi wa Nasa Raila Odinga kwa kuongoza wabunge wa muungano wa Nasa kuunga mkono mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta kuweka ushuru wa asilimia nane kwa mafuta, pamoja na bidhaa zingine muhimu.

Bw Odinga aliongoza mkutano wa wabunge wa Nasa katika makao ya Orange House Jumanne, ambapo aliwashurutisha kuunga mkono mapendekezo hayo, hata kama ni kwa masharti.

Lakini hatua yake hiyo imeishia kuwakasirisha mamilioni ya Wakenya, ambao ndio watabeba mzigo wa ushuru.

Mwanawe, Raila Odinga Jr alikuwa mmoja wa Wakenya wengi ambao hawakufurahishwa na hatua ya muungano wa Nasa, akieleza ghadhabu zake kupitia akaunti yake ya Twitter Jumanne.

“Kwa bahati mbaya kama raia wa Kenya sijaridhishwa na ujumbe wa Nasa kuhusu suala la ushuru wa VAT kwa mafuta, kati ya matakwa waliyoweka hakuna linaloweza kupimika n ahata kama yangepimika hayawezi kusaidia kuokoa mzigo wa deni. Naomba mbunge wangu @okothkenneth kupinga,” Raila junior akasema kupitia mtandao wake wa Twitter Jumanne.

Baadhi ya wafuasi wa Nasa walieleza Taifa Leo kuwa Bw Odinga aliwasaliti, kwani kwa miaka mingi ni yeye amekuwa mtetezi wa Wakenya masikini kutokana na kunyanyaswa na serikali.

“Ninahisi kuwa Raila na jeshi lake la Nasa wametusaliti. Wanawezaje kuunga mkono hatua inayolenga kutunyanyasa? Hii ndiyo sababu tuliwachagua?” akasema Bw Bramuel Omondi, mkazi wa Migori.

Alikosoa Bw Odinga kuwa amekuwa akidai kuwa anapigania mwananchi wa kawaida, akishangaa kwanini tena akachukua hatua ya kummaliza mwananchi.

“Hili suala la VAT sasa limetoa picha yake kuwa ni kibaraka na kama mfuasi wake nimeghadhabishwa sana,”akasema Bw Omondi.

Baadhi ya wafuasi walilaumu muafaka uliowekwa kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta kuwa umefunga mdomo upinzani kuzungumza dhidi ya maovu ya serikali.

“Ikiwa muafaka ulilenga kufanya Nasa sehemu ya serikali basi hautusaidii,” akasema Bw Hesbon Onyango, mfuasi wa Nasa.

Wakenya wengine kupitia mitandao ya kijamii walirejesha kumbukumbu za Bw Odinga alivyopinga vikali kuwekwa kwa ushuru wa VAT mnamo 2013, alipodai kuwa uchumi hauwezikukuzwa kwa kutoza wananchi ushuru.

“Tumemzoea Raila kuwa mtu anayesimama na watu wakati mgumu lakini siku za hivi majuzi hajakuwa thabiti katika masuala yanayomhusu mwananchi. Anaunga mkono serikali hata wakati inakosea,” Bw Onyango akasema.

Mnamo Mei 27, 2013 wakati sheria ya ushuru wa mafuta ilipitishwa, Bw Odinga alichapisha kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba “Uchumi hauwezi kukuzwa kwa kutoza ushuru” akipendekeza kuinuliwa kwa sekta za kibinafsi kujenga uchumi.

Aidha, Wakenya wengine wameshangazwa na Bw Odinga ambaye juzi aliwahakikishia kuwa Rais Kenyatta atatatua tatizo hilo la ushuru wakati ulipoanza kutekelezwa akiwa nje ya nchi.

“Msijali hata kidogo, Rais ataondoa ushuru huo wa bidhaa za mafuta kwani anasikiza kilio cha wananchi,” Bw Odinga akasema alipokuwa Kisumu.

Lakini sasa baada ya kuwa wazi kuwa Rais hana nia ya kufanya hivyo, Wakenya wengi wameishia kumlaumu Bw Odinga ambaye sasa wanasema ametiwa mfukoni na Rais Kenyatta ndio maana ananyamaza maovu yakitendeka.