Habari Mseto

Wakenya wanaoishi Amerika waunga Biden kuchaguliwa

November 3rd, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA akiwa Amerika

WAKENYA wengi wanaoishi Amerika wanamuunga mkono mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden kuwa Rais kwenye uchaguzi unaofanyika leo Jumanne.

“Ikiwa unajali maisha ya baadaye ya wanao unaowalelea hapa Marekani, haidhuru hata ukikosa kwenda kazini angaa siku moja ili ushiriki uamuzi huu muhimu,” akasema Bi Jane Wanjiru.

Hata hivyo, wapo wachache kama Macharia wa Manyeki wanaomuunga mkono Rais Donald Trump wa chama cha Republican.

“Rais Trump aliwekwa hapo na Mungu ili kunyoosha mambo na kuirejeshea nchi hii hadhi ya miaka mingi iliyofifishwa na Rais Obama,” Bw Manyeki anakariri.

Lakini kauli hiyo imewaudhi Wakenya wengi: “Ni aibu iliyoje kumsikia Mwafrika, hasa Mkenya, akimuunga mkono Trump ilhali anahatarisha haki yetu ya kuishi huku? Tukipokonywa uraia, hata hao wanaomuunga mkono hawataachwa nje. Jameni tumchagueni Biden,” akaandika Dkt Frank Karani.

Bi Alice Otieno alisema alimpigia kura Biden wiki jana, ingawa alifanya hivyo shingo upande: “Wajua, mimi ni Mkristo. Masuala ya uavyaji mimba na mapenzi ya jinsia moja yanaoungwa mkono na Democrat yaliniwia ugumu moyoni. Hata hivyo, Ukristo anaodai kuzingatia Trump sio ninaojua. Kuna unafiki mwingi katika uchaguzi huu.”

Bw John Kisavi anamuunga mkono Biden: “Tunatumaini kwamba, Biden atashinda. Tunahitaji uchaguzi wa amani. Demokrasia hapa Amerika imo hatarini.”

Wakili maarufu wa masuala ya uhamiaji, Bi Regina Njogu, ana wasiwasi kwamba mambo yatakuwa magumu kwa wateja wake ikiwa Trump atashinda: “Trump anataka kupokonya watu manufaa ya uhamiaji. Pia anataka kuondoa kabisa ile bahati nasibu ya Green Card ambayo ni njia kuu inayowaleta Waafrika wengi Amerika.”

Naye msomi Dkt Jane Waithira amesema kwa tahadhari: “Sitasherehekea hadi nione Biden ameshinda majimbo ya Florida, Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Nevada na Arizona.”

Hata hivyo, wapo wanaoamini Biden atashinda, hivyo mustakabali wa maisha yao kwenye nchi ya watu hii utakuwa mzuri.

Naye Profesa James Ngundi wa Chuo Kikuu cha Georgetown, jijini Washington D.C., anaamini Trump atabwagwa, ila atajaribu kuzua msukosuko wa kikatiba ili asalie madarakani.

Kwa jumla, Wakenya wanahofia hali ngumu ya maisha iwapo Trump atashinda.