Habari Mseto

Wakenya wanaotamani kusafiri Canada waonywa

May 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA wametahadharishwa dhidi ya walaghai wanaouza visa feki kwenda Canada, na ahadi za kazi hewa nchini humo.

Kulingana na shirika la kimataifa ambalo hutoa visa, Wakenya wanapoteza kufikia Sh2.15 milioni kwa mtu mmoja kwa walaghai hao.

Lilisema hayo Jumatatu kuonya Wakenya wanaotafuta kazi nchini humo ili kujihadhari na walaghai hao.

Udanganyifu huo unalenga Wakenya wa mapato ya chini na pia wale wa mapato ya juu wanaotafuta kazi nchi za nje, lilionya shirika hilo katika taarifa.

Walaghai hao hupata Sh150 milioni kwa kuwapora watu 150 katika muda wa miezi miwili au mitatu.

Kulingana na Beaver Immigration Consulting, walaghai hao wamewaibia mamia ya Wakenya.

Bw Nicholas Avramis, ambaye ni afisa wa Beaver Immigration Consulting, shirika hilo limekata tamaa kuhusiana na ongezeko la visa hivyo chini ya mpango huo.

“Nimevunjika moyo kutokana na kuwa ninaendelea kupokea simu kutoka kwa watu waliolaghaiwa. Hili ni tatizo la kilimwengu kuhusiana na uhamiaji Canada. Visa kama hivyo ni vingi sana India na China ila sasa walaghai wameanza kufika Afrika kuibia watu,” alisema Bw Avramis.

Walaghai huahidi waathiriwa kuwa watawapa visa wakifika Canada ili kuwa na uwezo wa kufanya kazi, au idhini wazi ya kufanya kazi humo, ambayo haipo kwa watu wasio raia wa Canada, alisema afisa huyo.

Wengine huwadanganya waathiriwa kuwa wana uwezo wa kuwatafutia kazi kwa kuwahifadhia barua ya ajira kutoka kwa kampuni za Canada.