Habari Mseto

Wakenya wanapenda minofu ya kuku kuliko nyama ya ng'ombe – Ripoti

September 19th, 2019 2 min read

Na CAROLYNE AGOSA

WAKENYA wengi wanapenda nyama ya kuku zaidi kuliko ya ng’ombe. Aidha, samaki wamekuwa maarufu zaidi kuliko nyama ya mbuzi.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya utafiti kuhusu ulaji nyama katika kanda ya Afrika Mashariki, nyama ya kuku ndiyo maarufu zaidi miongoni mwa Wakenya kwa asilimia 93.

Nyama ya ng’ombe inafuata kwa asilimia 85 nayo samaki ikichukua nafasi ya tatu kwa asilimia 79.

Tafiti za awali husema, wengi wanakumbatia nyama ya kuku kwa sababu ya jinsi imebainika nyama nyeupe ni bora zaidi kwa afya ikilinganishwa na nyama nyekundu.

Kuku hupatikana kwa urahisi zaidi kuliko samaki ambayo pia ni nyeupe, na pia wengi huwa hawapendi kula samaki.

Walaji nyama ya mbuzi wako katika nafasi ya nne kwa asilimia 76 huku nyama ya nguruwe ikifunga orodha ya tano bora kwa asilimia 51.

Ripoti hiyo Consumer Perceptions on Animal Welfare and Food Safety across East Africa, imetayarishwa na shirika la World Animal Protection.

Wakazi 1,346 wenye umri wa miaka 15 na zaidi walihojiwa katika miji mikubwa ya Afrika Mashariki.

Utafiti huo ulifanywa nchini Kenya, Tanzania, Uganda na Zambia. Vile vile, watu kadha walihojiwa Afrika Kusini, Nigeria, Misri, Namibia, Brazil, Msumbiji na Rwanda.

“Wananchi Afrika Mashariki wanakula nyama ya kuku kwa wingi – asilimia 93.1. Nyama ya ng’ombe inafuata kwa asilimia 84.3, mbuzi asilimia 72, samaki asilimia 76, nguruwe asilimia 57.3, kondoo asilimia 34.6 na sungura asilimia 21.0,” alisema msimamizi wa utafiti huo, Dkt Victor Yamo katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Nairobi.

Licha ya nyama ya kuku kuwa maarufu zaidi, Dkt Yamo alisema gharama yake ya juu imefanya wengi kula siku maalum pekee, kama vile wakati wa sherehe.

“Aidha, ingawa karibu nusu ya wananchi wanapenda kula nyama mchana (asilimia 46.1), mmoja kati ya watatu hula nyama wakati wowote ule – asubuhi, mchana, jioni, usiku na kadhalika!” aliambia kikao.

Kwa ujumla, wananchi wa Tanzania ndio wanapenda kula nyama sana (asilimia 50.5). Kwa upande mwingine, wananchi wanaokula nyama kwa vipimo wanapatikana Uganda (asilimia 64.5), Kenya (asilimia 59.8), na Zambia (asilimia 51.2).

Wananchi wengi wanaamini sana nyama ya bucha kwa asilimia 65.2 huku asilimia 20.7 pekee wakinunua nyama yao kutoka kwa maduka makubwa ya jumla.

Alieleza Dkt Yamo: “Sababu kuu ni kwamba maduka hayo yako karibu na nyumbani, vyakula ni salama na yauzwa kwa bei nafuu.”