Makala

Wakenya wanateseka katika magereza ya ughaibuni bila usaidizi – Monica Juma

October 3rd, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa Wakenya hawapati usaidizi kutoka kwa afisi za kibalozi za Kenya katika mataifa ya ng’ambo baada ya ripoti kuwa idadi kubwa wanateseka katika magereza katika mataifa kadhaa ulimwenguni.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa bungeni Jumanne na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Monica Juma jumla ya Wakenya 273 wanazuiliwa katika magereza katika mataifa ya kigeni kwa makosa mbalimbali.

Taifa jirani la Tanzania ndio linaongoza kwa kufungia idadi kubwa ya Wakenya ambayo ni 79 kulingana na stakabadhi ambayo Bi Juma aliwasilisha mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni.

Miongoni mwa Wakenya hao ni mfanyabiashara Don Bosco Gichana ambaye aliachiliwa baada ya kuzuiliwa katika gereza moja jijini Arusha kwa makosa ya ulanguzi wa pesa na kupanga njama ya kutekeleza uhalifu.

Bw Gichana ambaye pia ni mwanasiasa, aliachiliwa huru baada ya kulipa faini ya Sh13.2 milioni

Dkt Juma pia aliiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kajiado Kusini Katoo Ole Metito kwamba Kenya haiweza kumudu mpango wa kuwatetea Wakenya hao ambao wanateseka katika magereza ya ng’ambo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni Monica Juma alipofika mbele ya kamati Oktoba 2, 2018. Picha/ Charles Wasonga

Hata hivyo aliwahimiza Wakenya wanaoishi katika mataifa ya kigeni kujisajili na Balozi za Kenya katika mataifa hayo ili wapewe “huduma za kimsingi”.

“Hatuna mpango w kuwasaidia watu wetu wanaokamatwa ng’ambo kwa tuhuma mbalimbali kwa sababu mpango huo unaojumuisha ukodishaji wa mawakili wa kimataifa ni ghali mno.

Kile tunafanya ni kuwahimiza Wakenya katika mataifa ya ng’ambo kuheshimu sheria za huko,” Dkt Juma akasema huko akiahidi kutoa takwimu kamili ya Wakenya walioko katika magereza ya ng’ambo baada ya majuma mawili.

Vile vile, waziri huyo alisema maafisa wa balozi za Kenya katika mataifa ya nje wameagizwa kushauriana na Wakenya wanaoishi huko kila mara ili kuzui uwezekana na Wakenya hao kuvunja sheria na kuishia kukamatwa.

Kulingana na takwimu ambazo Dk Juma aliwasilisha kwa kamati hii, China ina wafungwa 57 wa asili ya Kenya, Uganda (47), Malaysia (25), Sudan Kusini (10), Qatar (8), Thailand (7), Ushelisheli (6), Ethiopia na Indonesia (5), Ufilipino, Kuwait, Botswana na Pakistan (3 kila mmoja) huku mataifa ya Togo, Oman, Afrika Kusini (2 kila mmoja). Rwanda, Japan, Australia, Brazil, Nepal na Korea Kusini, kila moja ina Mkenya mmoja katika magereza yake

Hata hivyo, Waziri huyo alisema sheria inayozuia ufichuzi wa data katika mataifa ya Uingereza na Uswizi inazizuia kutoa idadi ya Wakenya wanaozuiliwa katika magereza yazo. Maelezo kuhusu makosa yao pia hayawezi kutolewa.