Habari

Wakenya wanavyotumia ujanja kuingia na kutoka Nairobi

April 8th, 2020 2 min read

JUMA NAMLOLA, JOSEPH OPENDA, SIMON CIURI Na JOSEPH NDUNDA

WAKAZI wa kaunti zinazopakana na Nairobi na viunga vyake wamelazimika kuvumbua ujanja wa kuingia na kutoka jiji kuu kufuatia marufuku iliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumatano.

Rais Kenyatta alitangaza marufuku pia katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale, ambazo pamoja na Nairobi zimeandikisha idadi kubwa ya watu waliothibitishwa kuugua virusi vya corona.

Kwenye marufuku hiyo, Rais alisema watu hawataruhusiwa kutoka ama kuingia katika kaunti hizo nne ili wasisambaze maradhi hayo kwingineko.

Lakini Jumanne, watu waliokuwa wakitaka kwenda kaunti za Mlima Kenya walikuwa wakifikishwa na magari katika Daraja la Chania mjini Thika baada ya polisi kuwalazimisha kushuka na magari kukatazwa kuendela na safari.

Kisha walikuwa wakitembea umbali kiasi na kubebwa kwa bodaboda ambazo ziliwasafirisha mbele ambako walipanda magari ya kuwapeleka maeneo waliyokuwa wakitaka kufika.

Hii ni kwa kuwa baada ya kuingia Kaunti ya Murang’a walikuwa na uhuru wa kusafiri hadi kaunti zingine zisizo na marufuku, licha ya kuwa walitakiwa kukaa Nairobi.

Kaunti ambako wangeweza kufika baada ya kuvuka Mto Chania ni Kirinyaga, Embu, Nyeri, Laikipia, Isiolo, Marsabit, Meru na Tharaka Nithi.

Pia wangeweza kupata usafiri hadi maeneo ya chini ya Machakos kupitia Embu, ama hata kwenda Nyandarua na Nakuru kupitia Nyeri na kutoka hapo maeneo mengine.

Hali ilikuwa sawa kwa waliotaka kuingia Nairobi na viunga vyake. Mmoja wa wasafiri, Bi Jemmimah Kanyi, aliambia Taifa Leo kwamba alilazimika kupanda bodaboda na kulipa Sh200 ili apelekwe Thika Mjini.

“Nilitoka Kandara kwa matatu lakini tukashukishwa kwenye shamba la Del Monte. Nilikuwa naenda kuona daktari mjini Thika. Polisi walitwambia Rais Kenyatta aliagiza kusiwe na safari kati ya kaunti zinazopakana na Nairobi,” akasema Bi Kanyi.

Polisi wa kupambana na ghasia waliojumuisha kikosi cha GSU, walikuwa wakali kiasi kwamba kwa waliokuwa na magari hata mwanajeshi wa KDF aliyesema alikuwa akirejea kazini kutoka likizo walikatazwa kupita.

“Nimefika hapa saa tatu asubuhi nikitoka likizoni Embu. Sasa ni saa nane sijafanikiwa kuwashawishi maafisa hawa,” akasema.

Hata hivyo, baadaye aliruhusiwa kuendelea na safari baada ya kuwapigia simu wakuu wa jeshi jijini Nairobi.

Bi Charity Mwaura aliyeonekana mnyonge baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitali mjini Thika, aliambia Taifa Leo wasiwasi wake mkubwa ulikuwa ni jinsi ya kufika kwake.

Katika mpaka wa Machakos na Nairobi, watu walitumia njia za mkato kupitia Mto Athi kuingia na kutoka jiji kuu.?“Walilkosa kufunga uwanja wa ndege, wakaruhusu wageni kutuletea corona. Sasa wanataka kutuzuia kwenda kujitafutia riziki? Lazima tutafute mbinu za kufika kazini kwetu,” akasema mmoja wa wanaume waliotumia njia hiyo ya mkato.

Kwenye mpaka na Rift Valley, Mshirikishi George Natembeya aliwaonya wakazi wenye nia ya kukiuka marufuku hiyo kuwa watachukuliwa hatua kali.

“Tumewatuma maafisa wa usalama kwenye barabara zetu na kuwaagiza wasiruhusu gari lolote la uchukuzi kutoka Nairobi hadi eneo hili. Magari yote yanayotoka Nairobi yataamrishwa yarejee huko,” akasema afisa huyo wa utawala.

Mnamo Jumatano jioni baadhi ya watu walikesha kwenye baridi eneo la Kamulu kwenye barabara ya Kangundo inayoelekea Machakos, baada ya polisi kuwakataza kupita wakitoka kazi na biashara Nairobi.

Hii ilibidi Waziri wa Usalama Fred Matiang’i jana kuandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na kusongesha mpaka wa Nairobi na Machakos kutoka Kamulu hadi Koma.