Makala

Wakenya wanavyotumiwa kama maajenti kulangua dawa za kulevya

March 24th, 2024 3 min read

NA BENSON MATHEKA

VITA dhidi ya dawa za kulevya vinapoendelea kupamba moto nchini, ripoti zinaonyesha kwamba huenda Wakenya wanatumiwa kama maajenti wa ulanguzi wa mihandarati.

Hii ni baada ya kuibuka kuwa Kenya imekuwa ikitumiwa kama kituo cha kupitishia dawa za kulevya hadi mataifa mengine.

Na kwa miaka mingi Serikali imelaumiwa kwa kutochukua hatua kuzima ulanguzi wa dawa hizo.

Kulingana na ripoti moja ya shirika la kimataifa la kudhibiti dawa za kulevya (INCB), walanguzi wa mihadharati kutoka bara Asia wamekuwa wakitumia Kenya kama kituo cha kusafirisha dawa haramu hadi nchi za bara Ulaya.

Shirika hilo linataja dawa aina ya Heroin kama iliyo maarufu miongoni mwa zile zinazopitishiwa Kenya hadi mataifa mengine.

Kulingana na INCB, Kenya pia imekuwa ikitumiwa na walanguzi wa mihadharati kutoka Afghanistan.

Shirika hilo lasema kuwa matumizi ya dawa hizo nchini yaliongezeka kwa sababu baadhi ya yanayonuiwa kupelekwa kwingine hupata soko nchini.

“Matumizi ya mihadharati hasa Heroin yaliongezeka Kenya kwa sababu nchi hiyo imekuwa ikitumiwa kama kituo cha kusafirisha dawa za kulevya hadi mataifa ya bara Ulaya na Amerika,” yasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inataja Nairobi na Mombasa kama miji inayotumiwa kusafirisha dawa hizo.

“Miji ya Kenya, hasa Nairobi na Mombasa kuliko na viwanja vikuu  vya ndege vilivyo na shughuli nyingi imekuwa  kivutio cha walanguzi wa dawa za kulevya,” alieleza  Bw Stefan Liller, aliyekuwa mkuu wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na dawa za kulevya na uhalifu, UNDOC wakati huo.

Kulingana na UNDOC, ufisadi umekuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.

Moja katika ya kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kunaswa nchini kilikuwa tani 1.1 zilizotwaliwa zikiwa zimefichwa katika jumba la kifahari mjini Malindi na mtaani Embakasi, Nairobi.

Kufuatia kunaswa kwa dawa hizo washukiwa wakuu, David Mugo, Tansukhal Thanki Estelle Duminga na Angelo Ricci mmiliki wa nyumba zilizofichwa walitiwa baroni.

Dawa hizo zilizokisiwa kuwa za thamani ya Sh13 bilioni ziliteketezwa baada ya mvutano mkali baina ya maafisa wa usalama, mashirika ya kijamii na wizara za serikali.

Ilidaiwa kuwa sehemu ya dawa hizo iliuzwa kwa njia isiyoeleweka zikiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Hata hivyo, maafisa wakuu serikalini na idara ya polisi walikanusha madai hayo.

Hofu ni kwamba Wakenya wamekuwa wakishiriki ulanguzi wa dawa za kulevya kama maajenti wa raia wa nchi zingine.

Inaaminika kuwa Wakenya wengi wamekuwa wakishiriki biashara hii haramu wakiwa maajenti wa raia wa Nigeria na nchi zingine za magharibi mwa Kenya.

Na hili ni tatizo lililodumu kwa miongo mingi.

Kwa mfano, 2005, polisi wa Uingereza waliwapatia wenzao wa Kenya majina ya washukiwa 40 wa dawa za kulevya waliokuwa wakitumia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Na idadi ya Wakenya wanaoshtakiwa katika nchi za kigeni kwa kulangua dawa imekuwa ikiongezeka jambo linalotilia mkazo jinsi uovu huu ulivyokita mizizi nchini.

Afisa mmoja katika Wizara ya Mashauri ya nchi za kigeni aliyeomba tusichapishe jina lake kwa sababu sio msemaji rasmi wa wizara, alikiri Wakenya walihusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Hatuwezi kukanusha kwamba Wakenya wamekuwa wakishiriki biashara hii kwa sababu baadhi yao wamewahi kukamatwa na kushtakiwa katika nchi za kigeni. Hata hivyo, wahusika wakuu wanaofanya biashara hiyo bado wako huru. Hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa ikiwa vita hivi vitafua dafu,” akasema afisa huyo.

Alitoa mfano wa wanafunzi wawili waliokamatwa na polisi mjini Kuala Lumpur, Malaysia mnamo 2002 wakiwa na kilo nne za dawa za kulevya.

Wanafunzi hao, Deborah Donde na Emily Gathoni walishukiwa kulangua marijuana, iliyoorodheshwa kimataifa miongoni mwa dawa hatari za kulevya.

Januari 20 2024, mwanamke Mkenya mwenye umri wa miaka 26 alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kempegowda, India kwa kulangua kilo 2.6 za cocaine ya thamani ya Sh13 milioni.

Bi Olivia Munoko, aliyekuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi hakuwa na bahati aliponaswa na kilo 1.8 za heroin mjini Guangzhous, Uchina mnamo 2006.

Mahakama ilimfunga maisha jela. Inaaminika kuwa walanguzi wa dawa wamekuwa wakitumia huduma za wanawake na hasa wanafunzi wa vyuo vikuu kusafirisha dawa hatari.

Mnamo 2002, mwanamke Mkenya, Bi Settena Idris Abdalla, alifungwa jela miaka 20 na mahakama moja  nchini Mauritius kwa kupatikana na kilo moja ya heroin.

Wakenya 150 wamewahi kunaswa kote ulimweguni wakisafirisha dawa za kulevya.

Mnamo 2001, Bi Emily Barasa, aliyekuwa mfanyikazi wa  kampuni ya Kenya Airways alinaswa na kifurushi kilichokuwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa Heathrow, London. Emily alitumika kifungo na kurejea nchini.

Mwaka mmoja baadaye, Bi Dorothy Manju Nzioki na Susan Kaluki, walizuiliwa na kitengo cha kupambana na dawa za kulevya nchini Amerika kwa madai ya kuingiza dawa hatari nchini humo.

Na mnamo 2005 Bw Allan Choge alitiwa mbaroni katika uwanja wa ndege wa Heathrow, London kwa kujaribu kuingiza kilo 5 za kokeini nchini Uingereza.

Mwaka huohuo, Bi Nancy Waiguru, aliyekuwa mtumishi wa shirika la ndege la Kenya Airways alinaswa katika uwanja huo huo kwa kupatikana na kilo 5 za kokeini zilizofichwa katika mkoba wake.

Waiguru alimaliza kutumikia kifungo cha miaka mitano mwaka jana, 2023. Kunaswa kwake kulifuatia kukamatwa kwa Bw George Kiragu mjini Amsterdam,  Uholanzi kuhusiana na  kilo 295 za kokeini zilizopatikana  zimefichwa katika eneo la Champagneweg 11 Te Zevenbergen jijini Amsterdam.